MAMA aliyemsaidia mwanawe kubaka , Regina Kigelulye,
ametupwa jela miaka 30 sawa na mtoto wake ambaye alikuwa anakabiliwa na kosa la
kubaka, Sagimembe Mroso.
Mtoto huyo pamoja na kwenda jela miaka 30
amepewa adhabu ya kuchapwa viboko 12, sita akiingia jela na sita
akitoka.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya
Mpwapwa, Paskal Mayumba mwendesha mashitaka wa Polisi Godwin Ikema alisema
watuhumiwa hao Sagimembe Mroso na mama yake Regina Kigelulye, wakazi wa mtaa wa
Hazina mjini Mpwapwa, Machi 6, 2014 walikula njama ya kumbaka Belita
Ndahani.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa namba moja Sagimembe
Mroso alifanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 130(A) na kifungu kidogo 2 na
kifungu 131(1) na sheria namba 16 ya kanuni ya adhabu.
Aidha ilidaiwa kwamba mshitakiwa wa pili Regina
Abdalah Kigelulye alimsaidia mwanawe huyo kufanikisha tukio hilo kwa kufunga
mlango kwa nje ili mwanamke huyo ashindwe kutoka nje.
Kitendo hicho kilielezwa kuwa kinyume na kifungu
namba 22 kifungu kidogo cha 1 na sheria ya kanuni ya adhabu namba 16.
Mayumba aliiambia Mahakama kuwa siku ya tukio
Regina akiwa muuguzi katika hospitali ya Benjamin Mkapa alimchukua Belita
Ndahani aliyekuwa akimuuguza baba yake katika hospitali hiyo na kwenda kulala
nyumbani kwake na ndipo alipomfungia mlango kwa nje na mwanawe huyo wa kiume
huku akimsihi yeye ni mtu mzima hivyo asipige kelele ndipo alipomwingilia
kinyume na ridhaa yake.
Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kwamba mama huyo
hakuridhika na kitendo hicho akawa anapiga makelele na majirani walipoulizia
kelele hizo waliambiwa kwamba mama huyo alitoka kijijini hivyo alikuwa anaogopa
watu aliokuwa anawaona ndani ya luninga.
Hata hivyo maswali yalipoongezeka alimfungulia
mlango na kumuamuru mwanawe amsindikize hospitalini kwamba alipofika korongoni
alimbaka tena.
Pia aliiambia Mahakama kuwa kutokana na
kumbukumbu zilizopo zinaonesha kuwa mtuhumiwa anaishi na virusi vya Ukimwi
hivyo alimbaka mama huyo bila kutumia kinga na kumhatarishia kupata maambukizi
na yeye.
Aliongeza kuwa hospitali ilimwanzishia na kwamba
mama huyo amepima mara kadhaa lakini imeonesha kuwa hana virusi vya Ukimwi.
Hata hivyo alisema kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho mumewe alimfukuza
nyumbani na mgonjwa wake ambaye alikuwa ni baba yake alifariki dunia sasa
ameathirika kisaikolojia.
Akitoa hukumu Hakimu Mayumba alisema kwamba kwa
mujibu wa kifungu namba 22 kidogo 1 (C) kinachosema atakayesaidia kufanikisha
uharibifu kutendeka au kwa kutazama kuwa mazingira yako salama adhabu yake ni
sawa na aliyetenda kosa hilo, alimtupa jela miaka 30.
Wakijitetea kabla ya hukumu mshitakiwa wa kwanza
(mtoto) aliomba Mahakama impunguzie adhabu kutokana na kuwa yeye ana watoto
watatu na anaishi na virusi vya Ukimwi.
Mtuhumiwa wa pili aliiambia Mahakama kuwa yeye
ni mzee ana miaka 60, pili ana watoto 10 wakiwemo watoto yatima ambao anawalea
yeye, pia ana ugonjwa wa shinikizo la damu hivyo aliiambia Mahakama impunguzie
adhabu.
Hata hivyo Hakimu Mayumba akitoa maelezo alisema
mashahidi na vielelezo vilivyofika mahakamani vimewatia hatiani watuhumiwa hao
na kwa kuzingatia sheria kifungu na 130 (1) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu,
mtuhumiwa namba 1, Sagimembe Mroso alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30
jela na kuchapwa viboko 12.
Aidha mtuhumiwa namba 2, Regina Kigelulye kwa
kuzingatia kifungu 22 kifungu kidogo (1)C na sheria namba 16 ya kanuni ya
adhabu Mahakama ilimtupwa jela miaka 30.
Pamoja na dhabu hiyo Mahakama iliagiza mali zao kupigwa
mnada kulipa fidia ya Sh milioni 5 kama sehemu ya fidia ya kudhalilishwa,
kumpoteza baba yake, na kupoteza ndoa yake kwa Belita Ndahani. Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment