Inaonekana kila kitu ni feki siku hizi.. SIRI ya mafanikio ya Padri feki, Josephat Asenga,
aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki kwa
kufuata taratibu zote maalumu bila kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga aliyetumia vitambulisho feki,
alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria
Madeko mkoani Morogoro, alipopewa fursa ya kuongoza Misa, alitekeleza wajibu
huo wa kipadri bila kuacha shaka.
Alivyojitambulisha
Akizungumza na Habari Leo jana, kiongozi mmoja
wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa), alithibitisha kuwa Asenga alipofika
Parokiani hapo kati ya Mei na Juni mwaka jana, hakutiliwa shaka hata kidogo
kuwa si Padri.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Asenga alifika
kanisani hapo akiwa amevaa mavazi ya kipadri na kujitambulisha kuwa yupo nchini
kwa mapumziko, akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo anakofanyia shughuli
zake za upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali na kuvalia mavazi ya kipadri, Asenga pia
alionesha kitambulisho na kusababisha uongozi uamini kuwa ni Padri na kumpa
makaribisho ya Padri mwenzao.
“Alipoonesha kitambulisho tulimwamini na jinsi
alivyokuja na mavazi ya upadri na muonekano wake alionao, haikuwa rahisi
kumtilia shaka,” alisema kiongozi huyo.
Kuongoza Misa
Baada ya kupata makaribisho ya kipadri, Asenga
kwa mujibu wa kiongozi huyo, aliomba apangiwe zamu ya kuongoza misa ya Jumapili
iliyofuata na kukubaliwa. Kiongozi huyo alithibitisha kuwa Asenga aliongoza
vyema misa hiyo, kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo kama zinavyofuatwa na
mapadri wengine.
Taratibu kwa kawaida Misa katika Kanisa la
Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu ambayo mapadri na waministranti, ambao ni
wasaidizi wao, huvaa majoho na kusali kabla ya kuingia kanisani wakisindikizwa
na nyimbo.
Baada ya kuingia madhabahuni, Padri hubusu
madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa. Mualiko huo hufuatiwa na
maelezo kidogo na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo waumini hutubu dhambi zao na
kujiweka tayari kusikiliza neno la Mungu.
Ibada ya kusomwa neno, kwa kawaida masomo matatu
kutoka vitabu vya Agano la Kale na Jipya katika kitabu cha Bibilia Takatifu,
Padri huanza kutoa mahubiri.
Mahubiri yakiisha, Misa huendelea kwa sadaka na
baadaye, Padri huongoza waumini kuanza kukumbuka maelezo ya siku ambayo Yesu
Kristo alitoa Sakramenti katika Chakula cha Mwisho kwa wanafunzi wake akitaka
wamkumbuke.
Kwa kawaida, eneo hilo ndipo Padri kwa mamlaka
aliyopewa, hufanya mageuzi ya sakramenti kuwa Hostia Takatifu, kwa maneno
mengine hubariki mkate kuwa Mwili wa Kristo na divai kuwa Damu ya
Kristo.
Kwa Wakatoliki, eneo la mageuzi ni eneo muhimu
na ndio waumini hutuma maombi kimya kimya, wakiamini ndio Kristo anashuka
mwenyewe.
Baada ya kutumikia Kanisa na kukubalika, Asenga
aliaga kuwa anarudi nchini Marekani kwa kuwa muda wake wa mapumziko, umekwisha
na kuagwa na Kanisa.
Taarifa tata
Wakati uongozi wa Kanisa Katoliki,
Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko, ukiwa na imani kuwa Asenga ni Padri na
amerejea New York, kuendelea na Utume, walipata taarifa za kushangaza kutoka
kwa baadhi ya waumini, wakidai wamekutana na Asenga mitaani.
Mbali na taarifa hiyo ya kukutwa mitaani na
waumini wake, taarifa zaidi zilieleza kuwa amekuwa akiishi na mwanamke katika
eneo la Ujenzi, kinyume na desturi za mapadri wa Kanisa Katoliki duniani, ambao
hawaruhusiwi kuoa.
Mtego 1
Baada ya taarifa hizo, kwa mujibu wa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, Asenga aliwekewa mtego na Paroko wa
Parokia hiyo ya Mtakatifu Maria Madeko, Malt Dyfrig Joseph.
Paroko huyo inadaiwa aliwaomba waumini
wamshawishi Asenga afike parokiani hapo na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko
huyo na kudai kuwa alipata upadirisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya Paroko huyo
kupata maelezo hayo, alifanya mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es
Salaam na kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Kukamatwa, akiri Mtego wa pili kwa mujibu wa
Kamanda Paulo, ulifuata kwa Paroko huyo kutoa taarifa Polisi kuhusu uwepo wa
Padri feki, ambaye aliaminiwa kwa kiwango cha kuruhusiwa kuongoza
Misa.
Taarifa hizo zinasema Alhamisi ya wiki hii, saa
10:30 jioni, Asenga alimpigia simu Paroko huyo na kuomba ampangie kazi ya
kuendesha Misa Jumapili ya leo parokiani hapo, na kukubaliwa ambapo Paroko huyo
alimtaka afike kanisani.
Baada ya kufika, taratibu za kujulisha Polisi
zilifanywa na askari walipofika kanisani hapo, walimkamata mtuhumiwa huyo. Kwa
mujibu wa Kamanda Paulo, baada ya kufanya mahojiano na Asenga, alikiri kuwa yeye
si Padri na walipokwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi, walimkuta akiwa na
majoho saba ya upadri.
Mikoani, mafunzo Taarifa zaidi zilizofikia
gazeti hili jana, zilibainisha kuwa Asenga huenda kwa kutumia mbinu hizo hizo,
alishaaminiwa kuongoza Misa katika mkoa wa Kilimanjaro katika maeneo ya Uru na
Moshi na mkoani Singida.
Mbali na kukubalika katika mikoa hiyo, lakini
taarifa zaidi zilibainisha kuwa Asenga alifanikiwa kote huko kuongoza Misa na
kuaminiwa, kutokana na mafunzo ambayo aliwahi kupata huko nyuma.
Inadaiwa Asenga alianza kupata mafunzo katika
Seminari ya Kanisa Katoliki ya Uru, ambako alipata mafunzo ya elimu ya
sekondari.
Baada ya kumaliza kwa mafanikio masomo yake
katika seminari hiyo, alichaguliwa kujiunga na Seminari ya Kibosho, ambayo
inatajwa kuwa maalumu kwa ajili ya kutoa elimu ya falsafa kwa wanafunzi na
wengi ni wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Mafanikio aliyoyapata katika masomo ya falsafa
katika Seminari ya Kibosho, yalimwezesha kujiunga na Seminari ya Kipalapala,
ambako inaelezwa ndiko kunakotolewa mafunzo ya Liturgia, ambayo nayo ni sehemu
ya mafunzo wapewayo wanafunzi wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Waumini Ingawa taarifa za mafunzo aliyopata
zinatiliwa shaka, lakini namna alivyoongoza Misa bila kutiliwa shaka,
imesababisha baadhi ya waumini kuanza kumjadili, ili kufahamu hasa nia yake
ilikuwa ipi.
Kutokana na taaluma nyingine aliyonayo ya
uhasibu, amesababisha baadhi ya waumini kuunganisha matukio na uwezo wake na
kuamini kuwa huenda hakuwa akitafuta sadaka.
Mmoja wa waumini aliyezungumza na gazeti hili
kwa sharti la kutotajwa jina, alidai kuwa huenda Asenga alikuwa na njama za
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wafadhili
mbalimbali.
Kwa mujibu wa madai ya muumini huyo, watu wa
aina ya Asenga, ambaye ana taaluma na uwezo wa kipadri, wana njia nyingi za
kujipatia kipato, hivyo inawezekana alidanganya wafadhili wake kuwa yeye ni
Padri ili apate ufadhili huo.
Muumini huyo alikwenda mbali na kudai huenda
masharti ya ufadhili huo, ni kupata picha au sauti yake akiongoza Misa
kanisani.
“Inawezekana kuna mahali aliomba ufadhili kwa
ajili ya kitu fulani na aliwadanganya kuwa yeye ni Padri, ndio maana akaamua
kuomba zamu ya kuongoza Misa.
“Utapeli umeingia mpaka kwenye nyumba za ibada
kweli? Wanadamu tumekosa hofu ya Mungu!” Alihoji muumini huyo na kuasa jamii
kuwa macho, kwa kuwa hivi sasa matapeli ni wengi na kila siku wanatoka na mbinu
mpya.
No comments:
Post a Comment