Thursday, January 29, 2015

NITAVUKAJE: Huyu anaendesha maisha kwa kufua nguo nyumbani kwa wateja wake

Ukisoma makala hii inaweza kukusaidia wewe au mtu unayemfahamu. Imeandikwa na Joyce Joliga

Kati ya wanawake ambao wanaamini kuwa mafanikio hayaji bila kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii ni Salome Sanga (58).

Salome ni mkazi wa Makambi katika Manispaa ya Songea na amekuwa akisifika kwa kufua nguo kwenye nyumba za watu mbalimbali zaidi katika Kikosi cha Polisi FFU na Kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania, Chandamali mkoani Ruvuma.

Mama huyo wa watoto wanane ambaye awali aliolewa mwaka 1973 na Aloyce Haule ambaye alizaa naye watoto watatu. Haule alifariki mwaka 1982 na miaka miwili baadaye, alifunga ndoa na Vitalis Mumba ambaye alizaa naye watoto sita na mmoja kwa bahati mbaya alifariki dunia hivyo kubaki akiwa na watoto wanane.

Anasema walitengana na Vitalis kwa kuwa hali ya maisha ilikuwa ngumu na kila kukicha alikuwa akipigwa na mumewe huyo ambaye hata hivyo alikuwa haihudumii familia yake.
“Niliachana naye nikaenda kupanga chumba na nilianza maisha  ya upweke nikiwa na wanangu wanne ambao tayari wameolewa wawili wako Dar es Salaam na wengine wawili Majengo Songea na wengine wanaendesha maisha yao vijijini.

Anasema anajivunia kufanya kazi hiyo ya kufua nguo katika nyumba za watu na wala hajutii kufanya kazi hiyo na hatishwi na maneno ya watu ambao hudharau kazi za watu.

Salome anasema kupitia kazi hiyo, imemsaidia kufahamiana na watu mbalimbali pamoja na kujipatia kipato kikubwa kinachomsaidia kuendesha familia yake bila msaada kutoka kwa ndugu zake ama jamii inayomzunguka.

Kwa sasa Salome anaishi na mama yake mzazi naye amezeeka pia  ni mgonjwa hivyo anamtegemea kwa mahitaji mbalimbali.
Anasema anaifanya kazi hiyo kutokana na kukabiliwa na dhiki kubwa na amekuwa akikabiliwa na matatizo mbalimbali, hivyo akaona njia ya kujikwamua ni kujishughulisha na kazi hiyo ili kupata fedha za kujikimu na kulipa pango la nyumba anayoishi.

“Unajua sikwenda shule kwa kiasi kikubwa, nimeishia darasa la saba, sasa ninatumia nguvu zangu kama mtaji,” anasema.
Anafafanua zaidi kuwa, kazi ya kufua nguo za watu ni ngumu ingawa inampatia kipato kikubwa.

“Nimekuwa nikikutana na vikwazo pamoja na  vitu mbalimbali ambavyo si vizuri kuvizungumza lakini bado sijakata tama…Nimekuwa nikiendelea kufanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa niwaridhishe wateja wangu,” anasema.

Anasema uaminifu ndiyo unaomfanya apate kazi nyingi na wakati mwingine anazikimbia kwa kuwa zinamwelemea.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wateja kutomlipa fedha zake kwa wakati , “Utakuta  umefua na ukimaliza kazi mtu anakukopa lakini nashukuru Mungu wengi ni waaminifu wamekuwa wakinilipa baada ya kumaliza kazi na wanaokuwa hawana pesa siku hiyo, wakitoa ahadi siku inayofata  wanaitekeleza,” anasema.

Anasema: “Changamoto nyingine ni kulipwa fedha kidogo tofauti na nguo za kufua na utakuta kwenye hoteli kubwa nguo moja mtu analipa Sh1,000 hadi Sh2,500 lakini kwa sisi tunaofua nyumbani wateja wetu wanatukadiria wenyewe utakuta anatoa rundo la nguo na kukupatia Sh7,000 basi huwa tunaridhika na kupokea.

Kutokana na kazi hiyo, anasema kwa siku anaweza kufua nguo katika nyumba tatu hadi nne kutegemea na upatikanaji wa kazi anazopata.

“Ninaanza kufua kwa kuanzia Sh3,000 hadi 15,000 na kujipatia pesa za kununua mahitaji yangu madogo madogo…,” anasema.

Anasema pamoja na kujishughulisha na kazi ya kufua nguo nyumbani  pia anajishughulisha na biashara ya uuzaji wa supu nyumbani kwake  eneo la Makambi na hata hivyo biashara hiyo haijampa faida kama inavyompatia  biashara ya kufua nguo nyumbani kwa watu.

Anasema kwa sasa anajitahidi kuendelea kufanya kazi yake ya ufuaji nguo kwa ufanisi mkubwa na anatamani siku moja kama Mungu atamjalia. Pia, akipata wafadhili wa kumjengea  nyumba ya kisasa ya kuishi  na ataweka mashine za kisasa za kufua nguo hivyo itamsaidia kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi ambao watakuwa wanahitaji huduma yake badala ya kuendelea kuzunguka kwenye nyumba za watu.



No comments:

Post a Comment