Mwananchi linaripoti kuwa....
Mwanamke aliyetambulika kwa jina la
Hawa Kundani amezua taharuki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, baada ya kuvamia ghafla na kupiga kelele akidai kutelekezwa na
mumewe ambaye ni Mbunge wa Dimani (CCM) visiwani Zanzibar, Abdallah Sharia
Ameir.
Tukio hilo la aina yake lilitokea
jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, na mwanamke
huyo akiwa ameongozana na mtangazaji wa kituo kimoja cha redio, Joyce Kiria aliingia
na kusababisha mshtuko kwa wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa dini ya
Kikristo waliokuwa wamealikwa hapo. Wakati huo walikuwa wakijadiliana suala la
Mahakama ya Kadhi.
Hawa akizungumza na gazeti hili
alidai kwamba Ameir ni mume wake walifunga ndoa mkoani Arusha mwaka 1999 na
kuzaa naye watoto wanne, lakini mmoja alifariki dunia.
“ Nashangaa amebadilika ghafla
amekuwa mtu wa kuoa wanawake na kuacha mara kwa mara, hadi sasa ameshaoa
wanawake wanne na kuwaacha mimi nipo tu, alinioa bado mdogo,” alidai Hawa.
Alidai kuwa watoto wengine wawili,
mkubwa ana miaka tisa na mwingine miaka sita walichukuliwa na mumewe huyo
akawapeleka kulelewa na mwanamke aliyemuoa jambo ambalo alidai linamuuma.
“ Naumia wanangu sijui wanaishi
vipi, huyu niliyembeba ni mlemavu, hamtaki amekuwa akininanga kwa maneno mengi
sana, mimi nimetoka naye mbali nilibadili dini kwa ajili yake, leo hii
ananitesa, hanitaki anipe haki yangu ili niishi mwenyewe,” alisema Hawa.
Kwa upande wa mbunge hiyo Ameir
alidai kwamba kesi yao ipo kwenye Mahakama ya Kadhi, akidai kwamba mwanamke
huyo amekuwa akimdhalilisha kwa kupitia mtoto huyo mlemavu ambaye alikiri ni
mwanaye.
“ Huyu ni mwanangu sishindwi
kumhudumia, lakini sitaki fedha ziende kwa huyu mwanamke atazitumia kwa mambo
yake mengine, mimi nilimpeleka kwa mama yake mzazi akakae naye huko lakini yeye
hataki,” alisema Mbunge Ameir.
Akizungumzia tukio hilo Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema ni tukio ambalo
limewafedhehesha kwa kuwa hawakulitarajia.
“Tulivamiwa na wanawake kama wanne
na wanaume wawili nafikiri mmoja alikuwa ni mpiga picha, mwanamke mmoja akawa
anapiga kelele, tulitaharuki kwa sababu maaskofu walikuwa wameanza kutoa maoni
yao,” alisema.
Alisema kwamba waliomba msaada kwa
maofisa usalama wa ukumbi na walifika na kuwachukua wahusika hao, kisha
kuwapeleka polisi kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment