Thursday, January 8, 2015

my article for newspaper: chumba cha kufulia

Umuhimu wa kuwa na chumba maalum cha kufulia ndani ya makazi yako


Nafahamu Watanzania wachache sana (labda na wewe ni mmojawapo) ambao wamejenga nyumba zao wakaweka chumba cha kufulia. Badala yake wanafulia nje na kwa ufinyu wa eneo baadhi utakuta dada wa kazi kakaa juu ya sakafu ya shimo la maji taka anafua, na hata wakati mwingine pakiwa na harufu mbaya lakini hana mahali pengine pa kufulia maskini. Au kwa baadhi ya wale wenye mashine za kufulia aidha wameziweka kwenye varanda uani au bafuni lakini sio kuwa pametengenezwa maalum kwa kufulia.

Baadhi hawataki kukubaliana moja kwa moja kuwa kuna umuhimu wa kuwa na chumba cha kufulia kwenye makazi yao. Lakini wewe mwenye nyumba utakapoamua kujumuisha chumba cha kufulia kwenye makazi yako ndipo utakapogundua ni nini ulichokuwa unakosa! Utakiona chumba hiki kama moja ya vyumba muhimu zaidi kwako.

Ni mazoea ya wengi kuwa na mahali pa kufulia “huko nje”  na lugha inayotumika ni peleka nje hizi nguo za kufua. Kwa miaka mingi kwa Watanzania walio wengi kuwa na  chumba cha kufulia kwenye makazi yao ni jambo lisilotiliwa maanani, limedharaulika au na pia kusahaulika, na mahali pa kufulia ni popote  tu hapo nyumbani ambako wewe mfuaji utakapoona panakufaa kwa wakati husika…iwe ni uani, juu ya karo la maji taka, chini ya mti na wakati mwingine bafuni.

Asante kwa teknolojia na utandawazi ambapo baadhi ya wenye nyumba wameanza kutenga chumba cha kufulia kwenye nyumba zao. Kwa miaka ya karibuni baadhi ya wenye nyumba na wajenzi wanatizama uwezekano wa kujumuisha chumba cha kufulia kwenye makazi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na eneo la kuhifadhia, sinki, uwezo ukiwepo mashine ya kufulia na bila kusahau mahali pa kunyooshea. Umuhimu wa sinki bado ni mkubwa hata kama utaweka mashine kwani si kila nguo itafuliwa kwenye mashine na pia kuna swala la kuloweka na kuosha viatu vyenye udongo.

Lakini haijalishi ni maridadi namna gani chumba hiki kinavyoonekana, jambo la msingi linabaki lilelile kuwa ni mahali pa mchakato mzima wa kubadili nguo chafu ziwe safi na kuvalika tena ambapo ni pamoja na kuloweka, kufua, kunyoosha na kuhifadhi kwa muda.

Je, unaonaje kama kwenye eneo la makazi yako iwe unajenga sasa au ni makazi ya zamani ukawa na chumba cha kufulia? Na je unafahamu kuwa unaweza kukidizaini mwenyewe? Chumba cha kufulia kina majukumu yote ya kufanya mchakato wa kufua nguo uwe rahisi, pia kumbuka ni muhimu kiwe jirani na kamba za kuaniakia.

Hakikisha kwenye chumba chako hicho maalum cha kufulia una mahali pa kutundika nguo na tumia hanger za plastiki, hizi zinafaa zaidi kwani hazipati kutu au kujikunja pale nguo inapokuwa nzito.

Kwa matumizi mazuri ya nafasi unaweza kujenga kaunta la zege juu ya mashine ya kufulia ambapo ndipo utakapokuwa unanyooshea nguo. Kwa maana hiyo mashine yako inabidi iwe ni ile ya kujazia nguo kwa mlango wa mbele (front load) na sio juu (top load). Hii itaokoa eneo ambalo ungeweka meza ya kunyooshea.

Msisitizo maalum uwekwe kwenye muundo wa chumba hiki kuhakikisha kuwa kila mahali kuna mwanga wa kutosha, kwa mfanyo huwezi kufua kwa mikono penye mwanga hafifu na pia huwezi kunyooshea pasipo na mwanga wa kutosha. Ikiwezekana kuweka mlango wa kioo ni njema zaidi.

Chumba cha kufulia kinafaa kiwe na mvuto! Rangi nzuri za mwanga ukutani kama bluu au njano isiyokoza itaongeza muonekano. Sakafu yake iwe kavu na pia chumba hiki hakitakiwi kuwa kimepooza. Kuweka chanzo cha burudani kama vile radio inaweza kukifanya kiwe sehemu ya burudani zaidi kuwepo na kutomchosha mfuaji wakati nguo zikiendelea kutakata.

Chumba chako cha kufulia kinatavyokuwa na mvuto huenda kikamfanya mwenzi wako asiyependa kufua aanze kufua. Na kama ndio hivyo, ni ukweli kuwa kinaweza kuwa chumba kizuri zaidi hapo nyumbani!


Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christinesdaughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment