Friday, January 23, 2015

Jinsi ya kujiweka mazingira bora ya mafanikio kimaisha (1)

Nimekutana na makala hii na nikaamini kuwa nikiiweka hapa wapo watakaojifunza kitu hivyo kuwawezesha kuvuka kwenda level ya juu, tunajifunza kila siku. Mwandishi wake ambaye ni Dr. Chris pia ni marriage cousellor

Na DK Chris Mauki

Mafanikio ya kweli ya binadamu yanahusisha maeneo kama  mafanikio ya kiuchumi, kama vile kuwa na uwezo wa kujikimu na kumudu gharama za maisha ya kila siku.
Tunapozungumzia mafanikio binafsi, tunalenga kwa upana maisha ya mwanadamu. Unaposema mafanikio, wengi wanaelekeza mawazo yao kwenye kuwa na fedha, nyumba, magari na utajiri.

Mafanikio ya kijamii ni kama vile kuwa na mahusiano bora na wanaokuzunguka.
Mafanikio ya kiroho ni kama vile kuwa thabiti kwenye mambo ya kiimani.
Mafanikio ya kihisia ni  kama vile kuwa na uwezo wa kujimudu kihisia na kadhalika.

Ili kujiwekea mazingira bora katika kuyaelekea mafanikio yetu binafsi ni vyema ufahamu na kuweza kufanya yafuatayo.
Kutambua umuhimu wa muda na jifunze kuukomboa na pia kuwa na malengo na kuyatumia katika kuyatekeleza.
Jambo hili ni lazima kufahamu kuwa kamwe huwezi kuukomboa muda kama hujui umuhimu wake. 

Labda tuuangalie muda katika mitazamo tofauti.
Mtazamo wa kiimani ama kiroho, kuukomboa muda kumezungumziwa ndani ya vitabu vitakatifu kwa namna mbalimbali.
Baadhi ya maandiko yanaonyesha kuwa hata ibilisi mwenyewe anatenda kazi akijua kuwa wakati wake ni mchache sana.

Maeneo mengine katika misahafu imeeleza kuwa kati ya hatua za juu za busara ya mwanadamu ni  kujua umuhimu wa muda na kuukomboa.
Tukiangalia mtazamo wa kimaisha, watu wengi wameshindwa kufikia malengo yao waliyoyatamani kwa sababu ya kufikiri kuwa muda upo tele na kwa hivyo wangeweza kufanya walichokitaka wakati wowote na wakisahau ukweli kuwa muda ni mchache katika kila tunachotaka kukifanya.
Wenzetu Waingereza wana msemo usemao “There is little time for everything” wakiwa na maana kwamba kila sekunde, dakika inapaswa kutumiwa vizuri.

Kwa kutofahamu umuhimu wa muda wengi wetu wamekuwa wakifikwa na kihoro pale wanapokaribia kustaafu maana hamna walichokifanya wakiwa kazini.
Mara nyingi ninawashauri watu kuanza kuelekeza mawazo katika ile siku ya kustaafu mara tu unapoajiriwa.

Ukisubiri uwaze na kujiandaa kustaafu muda mchache kabla utajikuta unachanganyikiwa. Hii itakuwezesha kuelewa umuhimu wa muda mdogo ulionao kazini na namna ya kuukomboa ili usije kukuathirika baadaye.
Ni vyema ukifahamu ukweli kuwa uko vile ulivyo na jinsi ulivyo kwa kulingana na vile unavyoutumia muda wako.

Tumia muda wako kuwekeza katika busara na ufahamu, mfano; shule na kazi.
Katika  kutafuta kuwa na busara ni  lazima kufahamu kuna wakati wa kila jambo chini ya  jua na  lahitajika kutendeka au kufanywa katika muda wake mwafaka.
Wengi wetu tumepata hasara katika miradi mbalimbali maana tumeshindwa kujua muda mwafaka wa kuanza au kumaliza shughuli fulani au biashara  fulani.


Wiki ijayo tutaendelea na mada hii ya jinsi ya kujijengea mazingira bora kwa maisha ya baadaye kwa kuingia sehemu ya pili ya ‘Jifunze kuongozwa na malengo.’

No comments:

Post a Comment