Wengi wameanzisha biashara kwa nia ya kuvuka kutoka level moja kwenda ya juu, soma hapa upate desa la kuweza kupaa katika biashara yako.
Katika hali ya kawaida siyo rahisi
kukumbuka kichwani kila aina ya muamala unaofanyika katika biashara.
Hii inatokana na ukweli kuwa kichwa
cha binadamu kina mambo mengi ya kuingia na kutoka kulingana na hali halisi ya
maisha ya kila siku. Kwa kuzingatia hali hii, ndiyo maana kuna umuhimu wa
kutunza kumbukumbu za biashara ili kuifanya iendeshwe kitaalamu. Kimsingi,
utunzaji wa kumbukumbu za biashara una faida zifuatazo:
Husaidia kulipa kodi stahiki kwa
taasisi husika kama vile TRA. Ikumbukwe kuwa nchi huendeshwa kwa kodi. Bila
kulipa kodi hakuna maendeleo na huduma za jamii. Pia, ili biashara iweze kukua
sharti ilipe kodi kulingana na ukubwa wake. Iwapo utalipa kodi kubwa kuliko
kipato chake, biashara hiyo itakufa. Hivyo, kumbukumbu za biashara husaidia
kuondoa malalamiko ya ulipaji kodi kubwa au ndogo kuliko hali halisi ya
biashara.
Pia, kusimamia na kudhibiti kiwango
cha bidhaa iliyopo na inayotakiwa kuwapo. Utunzaji kumbukumbu za biashara
husaidia kujua muda unaopaswa kuagiza bidhaa husika. Ni makosa katika biashara
kuishiwa bidhaa inayohitajiwa na wateja, kwani mjasiriamali anaweza kupoteza
wateja hao. Vilevile siyo vizuri kuwa na akiba ya bidhaa nyingi ambayo
hainunuliki. Tatu ni kujua kiasi cha fedha kilichopokelewa. Biashara yoyote ile
huingiza fedha ambazo hutumika katika kuendeshea biashara husika. Kwa kuweka
kumbukumbu sahihi za mauzo ya kila siku kunamsaidia mjasiriamali kujua kiasi
cha fedha kinachoingia kila siku, mwezi na hatimaye mwaka mzima.
Hata kujua kiasi cha fedha
kilichotumiwa na namna kilivyotumiwa. Fedha inayotokana na biashara hutumika
kwa mambo mengi. Baadhi yake ni kununulia/kutengeneza bidhaa zinazohitajika
katika biashara husika ikiwa ni pamoja na matumizi ya kawaida.
Kusaidia katika ukokotoaji wa
mahesabu. Ili kujua kuwa biashara husika ina faida au hasara sharti kuwapo
ukokotoaji wa mapato na matumizi. Kama mapato yatazidi matumizi biashara hiyo
itakuwa inaingiza faida. Kama matumizi yatakuwa yanazidi mapato basi biashara
husika itakuwa inaingiza hasara na hivyo kuelekea kufa.
Mathalan, kusaidia katika kutoa
uamuzi sahihi juu ya kipi cha kununua na kuuza. Uwekaji wa kumbukumbu za
biashara husaidia kujua bidhaa inayohitajika na ile inayotakiwa kuuzwa kabla
haijaleta hasara. Biashara huna na bidhaa nyingine ambazo hazinunuliwi kwa kasi
inayohitajika na hivyo kuzifanya kuwa katika hatari ya kuleta hasara katika
biashara. Kwa kutumia utaratibu wa kuweka kumbukumbu mjasiriamali ataweza
kuzibaini na kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya biashara husika.
Kutunza kumbukumbu ya miamala
inayofanyika kwa mikopo husaidia kuepuka udanganyifu wa baadhi ya watu. Pasina
kumbukumbu juu ya miamala inayofanyika kwa njia ya mkopo, kunaweza kusababisha
kutokumbuka nani anadaiwa na kwa kiwango gani. Pia, husaidia kukomesha tabia ya
baadhi watu ambayo hukana madeni pale wanapobaini kuwa mdai hakuweka kumbukumbu
yoyote yenye kuwabana. Aidha, kuepukana na matumizi mabaya ya fedha na hali ya
kutoaminiana katika biashara. Kama hakuna kumbukumbu sahihi za biashara ni
rahisi kutumia pesa vibaya. Biashara inaweza kuwa kama shamba la bibi ambalo ni
mali ya kila mtu. Uwazi, kwa sababu kila kitu huwa kiko bayana katika maandishi
ambayo pande zote mbili zimehusika.
Kujua kama biashara inaendeshwa kama
inavyotakiwa ili kuhakiki hesabu za mwaka.
Imeandikwa na Chiraka Muhura.
No comments:
Post a Comment