‘Mume kanikimbia kisa nazaa sana’
“Sitasahau siku niliyokimbiwa na mume wangu baada ya kumzalia pacha kwa mara
ya tatu mfululizo.” Hii ni kauli ya Salome Paul Mhando, mama wa watoto sita
ambao ni pacha, aliowazaa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka sita
iliyopita, wakipishana miaka miwili miwili.
Salome, alitelekezwa nyumbani na mumewe huyo baada ya kujifungua pacha kwa
mara ya tatu, huku wakiwa hawana sehemu maalumu ya kuishi, achilia mbali njaa
iliyotokana na umaskini wa kipato.
Baada ya kutelekezwa, msamaria mwema alijitolea kumhifadhi katika shamba
lake lililopo eneo la Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kabla ya
kupata msaada wa nyumba ya kuishi.
Mama huyo anayekumbuka tukio hilo kwa uchungu, anasimulia kuwa mumewe
aliyemtaja kwa jina moja la Ali, alimtoroka saa saba mchana na kumwacha akiwa
na pacha hao.
Anabainisha kuwa tukio hilo lilitokea baada ya familia hiyo kukaa na njaa
kwa siku kadhaa kutokana na umaskini wa kipato.
“Siku hiyo, ambayo tarehe yake siikumbuki, mume wangu alirudi nyumbani akiwa
tena hana chakula na kunieleza kuwa anaumwa. Nilipomwuuliza sasa tunafanyaje
kuhusu chakula, alitoka nje,” anaeleza mama huyo na kuendelea:
“Nikaamua kumfuata na kuanza kumsema nikimdai chakula. Baadaye (mumewe)
akaniuliza mbona unanisema? Mimi nikamjibu; naulizia masuala ya chakula,
tunafanyaje leo? Akasema; basi niache naenda kukitafuta.”
Salome anaeleza kuwa kinyume na ahadi hiyo, tangu wakati huo alipoondoka
hajaonekana nyumbani hadi sasa. “Niliamua kwenda kulala, lakini nikiwa na
wasiwasi kuhusu usalama wake. Nikapatwa na hofu nikijiuliza; nini kimempata
mwenzangu na kuanza kuwapigia simu ndugu zake ambao pia hawakupatikana.”
Salome anasema jitihada za kuwatafuta ndugu wa mumewe ziligonga mwamba na
hadi sasa hana mawasiliano yoyote na familia hiyo ya mumewe.
Anaeleza kuwa kutokana na mumewe huyo kutorudi tena nyumbani, alilazimika
kwenda kwenye vyombo vya habari kuomba msaada wa malezi ya watoto hao.
“Nilikwenda kwanza ITV ambako mbali na kunisaidia katika mahitaji ya msingi
ya chakula, walinitangaza pia kwenye luninga kuwa ninahitaji msaada na tukio
hilo ndilo limenisaidia kupata msaada wa kudumu.
Hali ikoje?
Salome anahusisha kutoroka nyumbani kwa mumewe na ugumu wa maisha unaoikabili
familia hiyo.
“Nina watoto pacha sita; wawili wana umri wa miaka sita, wawili wengine wana
umri wa miaka minne na wawili wa mwisho wana umri wa miezi 12. Nasikitika
kukimbiwa na mume kwa sababu ya ugumu wa maisha, lakini zaidi akidai kuwa
ninazaa sana. Maisha ni magumu na ninashukuru kwa misaada ninayoendelea kuipata
kutoka kwa jamii, hasa kupatiwa msaada wa nyumba ya kuishi na wanangu,”
anasema.
Akifafanua kuhusu ugumu wa maisha, Salome anasema ameshindwa hata kuwapeleka
shule watoto wake wakubwa... “Hakuna anayesoma, wote bado wako nyumbani.”
Msaada wa nyumba
Hata hivyo, ugumu wa maisha wa Salome umeigusa Benki ya Covenant ya jijini
Dar es Salaam, ambayo imejitokeza kumnunulia nyumba ya kuishi na watoto hao
eneo la Mabwepande.
Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Sabetha Mwambenja anasema mbali na msaada
huo, anatamani kuona mume huyo aliyemtelekeza anapatikana na kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Anasema benki yake ilitambua mahitaji ya mama huyo kupitia vyombo vya habari
na kuamua kumpa msaada wa kumnunulia nyumba ya kuishi yenye thamani ya Sh25
milioni, ambayo alikabidhiwa juzi.
“Tumemkabidhi, nyumba, tukamnunulia magodoro, vitanda vinne, mashuka na taa
za sola na familia nzima tumeikatia bima ya afya itakayowawezesha kutibiwa
katika hospitali yoyote inayotoa huduma kupitia bima hiyo,” anaeleza mkurugenzi
huyo.
“Sisi hatuna kitengo wala idara inayojishughulisha na matatizo ya jamii,
tumeguswa tu na tatizo la mama huyo aliyekimbiwa na mumewe sababu ya kumzalia
pacha. Natoa wito kwa benki nyingine na wadau mbalimbali wa maendeleo kuguswa
na matatizo ya jamii inayowazunguka na kusaidia pale inapowezekana,” anasema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Balozi Salome Sijaona
anasema baada ya kuona mateso aliyokuwa akiyapata mwanamke huyo kwa kukosa
makazi, chakula na mahitaji mengine ya kibinaadamu, waliona ni vyema kujitolea
kumsaidia ikiwa ni moja ya kutimiza majukumu yake kwa jamii.
“Tumeguswa na mateso aliyokuwa akipata Salome Mhando, yeye pamoja na watoto
wake, baada ya kutelekezwa na mumewe kwa kigezo ha kuzaa watoto pacha
mfululizo. Tuliguswa na kuamua kujitolea kumnunulia nyumba ambayo ataimiliki
mwenyewe,” anasema Balozi Sijaona na kuongeza:
“Nyumba hii tumemkabidhi pamoja na samani za ndani ambazo sasa zitamwezesha
kuishi maisha ya amani na furaha akiwa kama wanawake wengine na kufurahi pamoja
na watoto wake.”
Shukrani
“Ninaishukuru Benki ya Covenant kuniwezesha kumiliki nyumba yangu,
ninawashukuru na ninaomba waendelee na moyo huo wa kuwasaidia kina mama wenye
matatizo kama haya kwa sababu siko peke yangu,” alisema Salome na kuongeza:
“Kina mama tumekuwa na wakati mgumu katika ndoa zetu hususan katika masuala
ya uzazi. Ninawashukuru watu wote ambao walijitolea kunisaidia chakula na nguo
katika wakati wote nilipokuwa sina sehemu maalumu ya kukaa, hadi sasa
ninamiliki nyumba yangu.”
No comments:
Post a Comment