Fahamu haya
kabla ya kununua mwavuli wa kwenye bustani
Kwa
kawaida ya binadamu anafurahia zaidi akiwa amepumzika nje ya jengo, ndio maana
utaona kuwa sehemu nyingi za burudani iwe ni kwenye migahawa wengi wanapendelea
kukaa nje kuliko ndani. Ukishafungia watu ndani tu, wanahama kuelekea pengine
ambapo watakaa nje. Sasa basi ni nani asiyependa kuwa na wakati mzuri akiwa katika
mazingira ya nje ya nyumba yake? Imekuwa ni burudani kwa binadamu toka enzi kwa
hivyo kuwa tu na meza na viti kwenye bustani bila mwavuli hailipi.
Samani
za kwenye bustani zimetengenezwa na wataalam, na wao wanajua zaidi, kwa hivyo
nimewauliza ushauri na wakanieleza ni
aina gani za samani zinazotakiwa kwa matumizi ya wazi kwenye bustani na katika
makala hii tutatizama zaidi mwavuli wa kwenye bustani.
Mwavuli wa
kwenye bustani zaidi ya kutumika pia ni pambo eneo la nje ya nyumba Mwavuli huu
ni sahihi kwa kuwapa wenyeji na wageni kivuli siku za jua kali. Na zaidi ni
kuwa unaboresha afya, Aisha anaanza kueleza.
Kwanza
kabisa ni lazima kuwa makini sana na malighafi iliyotengenezea mwavuli. Mwavuli
wa kwenye bustani unatakiwa kuwa imara sana kwani unatumika nje ya nyumba. Unatakiwa
uwe imara vya kutosha kuhimili jua la kiangazi, mvua kubwa na upepe mkali.
Miavuli hii ni mikubwa
tofauti na ile ya kubeba mkononi na inapatikana kwa maumbo, rangi na vitambaa
mbalimbali.
Kuamua ni aina
gani ya mwavuli wa bustani utakufaa inakupasa uijue kwa undani ndipo unapoweza
kufanya uchaguzi. Eneo la kitambaa la mwavuli huu ni lile linalowakinga jua na
mvua wale walio chini yake. Mwavuli unafaa uwe wa kufunga na kufungua mithili
ya ule wa mkononi na fremu zake zipo za aluminiam, mbao na chuma. Mlingoti wa
mwavuli unene wake ni kati ya inchi moja hadi tatu. Vipande vya fremu vinavyoupa mwavuli umbo lake
na kubeba kivuli ukiwa umefunguliwa vinapaswa kuwa imara. Mbavu za mwavuli (zile
zinazoshikilia kitambaa) pia zinatakiwa ziweze kuhimili pepo za wastani hadi za
kasi. Kitako cha mwavuli kiwe na uzito wa kutosha kubeba sehemu yote ya mwavuli
iliyobakia. Ukifahamu sehemu hizi za mwavuli wa bustani itakusaidia kupata
mawazo ya kuweza kununua mwavuli sahihi na wenye vigezo na malighafi utakazo,
anasema Aisha.
Nunua mwavuli ambao
unatosha eneo unalotaka kufunika na kukupa kivuli unachotaka. Miavuli ya kwenye
bustani inasimama yenyewe, na pia haijalishi ni mtindo upi, rangi na ukubwa
miavuli hii inapatikana kwenye maduka yanayouza samani za bustanini, anasema
Aisha.
Miavuli ya
bustani inauzwa yenye milingoti ya kati ya futi 6 hadi 13 japo mzunguko wa kivuli
hauhusiani na urefu wa mwavuli. Mwavuli wa bustani mdogo sana haupendezi,
mkubwa unafaa zaidi japo unategemea na ukubwa wa eneo lako. Pima ukubwa wa
samani zako au eneo litakalofunikwa na mwavuli husika kabla ya kununua mwavuli
wenyewe.
Kwa unene wa
mlingoti, wateja wenye meza zenye tobo la mwavuli katikati wanapaswa kupima kwanza
ukubwa wa tundu kabla ya kuamua unene wa mlingoti ili kujiridhisha kuwa sio
dogo sana au kubwa zaidi. Miavuli mikubwa inahitaji uimara zaidi, na milingoti
yake inakuwa minene.
Hakuna ubishi kuwa kitambaa cha
mwavuli ndicho kinachoonekana zaidi. Wenye nyumba wengi wanapenda kuchagua
kitambaa hiki kwa kutizama rangi. Wengine hupenda kuoanisha rangi ya kitambaa hiki
na rangi nyingine za nje ya nyumba zao. Wakati hili nalo ni muhimu, wanunuzi
wanapaswa pia kuchagua kivuli cha mwavuli kuendana na malighafi za kitambaa.
Zaidi ya kuamua
rangi au michoro fulani ya kitambaa, chagua mwavuli wa bustani wenye malighafi
zitakazohimili matumizi yako, wapo ambao wanauweka mwavuli bustanini kwa
kipindi cha matumizi tu na wapo ambao mwavuli upo hapo kila siku hautolewi. Malighafi
na rangi ya kitambaa utakayochagua isiwe inapauka au kuota ukungu.
Utakapoweka
mwavuli wa bustani nje ya nyumba yako huenda ukabadili mfumo wa maisha wa mwenzi
wako akajikuta badala ya kwenda baa mnatengeneza nyama choma na kula hapo hapo
nyumbani!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari,
nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christinesdaughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment