worth reading again and again
Umeshawahi kutamani kuona kwa
haraka kile unachokitafuta? Je vitu vyako mara kwa mara viko hovyo hovyo
vimesambaa kila mahali? Kama ndivyo basi, jifunze jinsi ya kuweka mpangilio wa
vitu nyumbani kwako kwa kusoma amri hizi kumi tunavoelekezwa na mjasiriamali na
mbunifu wa ndani Bi Alma Said.
1.
Weka vitu vinavyofanana pamoja. “Unapopangilia
vitu vyako weka vinavyoendana pamoja ili kuleta mtiririko na mantiki. Kwahivyo
acha kuweka chochote popote, inaweza kusaidia ndani ya muda mfupi lakini
ikafanya eneo lote lionekane mvurugano.
2.
Fikiria kabla ya kununua. Kununua kwa mhemko ni kifo cha mpangilio
wowote. Unataka kununua kitu? Kinahitaji makazi. Kuwa na uhakika na mpangilio
wako kabla hujaleta chochote kipya nyumbani kwako. Inasikika kama msongo eeh?
Ndio, panga kabla ya kununua: hiki kitakaa wapi? Je una nafasi, kama majibu ni
sijui na hapana basi acha usinunue (jumlisha
na kuwa utakuwa umehifadhi hela yako).
3.
Kila kitu kina mahali pake, kiweke hapo. Kwa lugha nyingine ni kuwa na eneo kwa kila kitu. Zaidi ya kuweka vitu
mahali pake ni kuwa pia kila kitu kinatakiwa kiwe na mahali pake kabla
hujakiweka hapo!
Eneo kwa kila kitu kwa mfano ufuatao, eneo la:
Eneo kwa kila kitu kwa mfano ufuatao, eneo la:
Hiyo kalamu wakati ambapo huiandikii.
Waya za kuchaji kamera na simu
wakati ambapo hazitumiki.
Barua ambazo hazijasomwa.
Soksi ambayo mwenzake haonekani
anasubiriwa kutafutwa.
Vipeperushi na magazeti ambayo utasoma
utakapopata muda, na vitu vingine vingi vingi hapo nyumbani.
Unataka kufahamu ni vitu gani hapo
nyumbani vinahitaji eneo lake maalum? Anza kwa kutizama kwenye kaunta yako ya
jiko. Kama kuna chombo kipokipo tu ni kwa sababu hujakitafutia eneo maalum.
4.
Zishukuru kumbukumbu zako halafu ziage. Hapana, sikushauri ulitose hilo
gauni lako la harusi. Kumbukumbu nyingine ni muhimu mno na zinahitaji eneo
kwenye nyumba yako maisha (wengine hadi wanazikwa na magauni yao ya harusi).
Lakini hizo CD na mikannda ya filamu? Fikiria mara mbili kabla hujabaki na hiyo
kumbukumbu unayotaka kuhifadhi maisha.
5.
Weka nguo zako mbali. Ndio najua unaguna,
lakini fanya hivyo, hakuna msamaha kwa hili. Nguo sio za kuwepo kila mahali.
Tundika zilizo safi, kunja za kukunja, fua zinazotakiwa kufuliwa na loweka za
kuloweka. Mwisho wa hadithi. Mrundikano wa nguo ni janga la nyumba nyingi.
Kutumia muda mchache kila siku kushughulikia swala la kuweka nguo
panapotakiwa itafanya mahali unapoishi
paonekane nadhifu na hivyo kurahisisha maisha yako kwa muda mrefu.
6.
Tumia vikontena vilivyopo kwa lengo lingine pindi vimalizapo lengo moja. Kwa maana nyingine ni kuwa tumia kile ambacho tayari
unacho. Nimeona
watu wanaotumia vikopo vilivyoisha biskuti ama chokoleti kwa ajili ya
kuhifadhia vitu kama hereni na vipodozi.
7.
Weka kituo cha amri . Manake ni kwamba
kituo hiki ndicho kinachokaa vile vitu kama funguo, mifuko, yani vile vitu
ambavyo vinatumika mara kwa mara kwenye pilika za kila siku. Hutakuwa na haja
ya kutafuta ama kuanza kuuliza kama utakuwa na kituo cha amri nyumbani kwako.
8.
Weka ratiba ya siku. Na hakikisha
unaifuata. Ratiba ni uti wa mgongo wa mipangilio. Hakikisha kila siku unatenga
muda wa kurudisha vitu pale vinapotakiwa kuwa, faili ripoti za watoto za shule
na karatasi nyingine muhimu, tandika kitanda na kadhalika ni kuwa nyumba yako
itakushukuru. Kumalizia siku na nyumba yenye mpangilio ni kweli kuwa unajisikia
vizuri ajabu.
9.
Anza kidogo kidogo. Kama huna karama
ya kuweka vitu kwenye mpangilio anza kidogokidogo na vitu vidogodogo kama vile
hicho kituo cha funguo, taratibu utashika kasi na kufika hadi kwenye kabati za
nguo. Furahia kimpangilio kidogo unachoanzia ambapo kitakupa stamina ya kusonga
mbele.
10.
Usichoke. "Kumbuka
kuwa wewe ndio msimamizi wa nyumba na vitu vyako. Kama utaiambia akili yako
nataka kuishi mahali penye mpangilio, muda si muda haitajisikia kuchoka.
Umesongwa? Sawa, chukua mapumziko kidogo.
Sasa
msomaji wangu umeelimishwa juu ya amri kumi za kuweka mpangilio wa vitu
nyumbani, je wewe ni mmojawapo wa wale wenye vitu ambavyo havina makao bado? Niandikie
ukinijulisha ni kwa namna gani umefaidika na makala hii kwa kuvipa eneo vitu
hivyo leo!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba.
Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment