Ya walimwengu ngumu kuyaelewa..
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia mwanamke
mmoja, Sophia
Chambo (30), mkazi wa Mtaa wa Polisi, Kata ya Lizaboni
Manispaaya Songea, akituhumiwa kujihusisha na biashara ya kuuza binadamu kwa
wafanyabiashara kwa ajili ya zindiko.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma,Mihayo Msikhela, alisema Februari 17, mwaka huu
saa nane mchana, Sophia alikwenda kwa mtu mmoja (jina linahifadhiwa) kwa sababu
za kiusalama kuwa akitaka afanikiwe afanye zindiko kwa kutumia maiti.
Kamanda, Msikhela alisema pamoja na mtuhumiwa huyo
kutoa ushauri huo, bado alimtaka wafanye biashara na yeye, kwani angeweza
kumletea mwili wa mama yake mdogo (jina tunalo) mkazi wa mtaa wa Ruvuma ambaye
alikuwa na ugomvi naye.
Alisema alitaka alipwe sh.milioni 10 ili akamletee
maiti ya mama huyo ikiwa kwenye gunia.
Alisema mtu huyo alikataa kupelekewa maiti na badala
yake alimtaka apelekewe mtu mzima akiwa hai na kwamba kazi ya kumuua ataifanya
yeye kwa makubaliano ya sh. milioni 6.5.
"Ndipo mtu huyo alitoa taarifa Polisi, hivyo
kufanikiwa kuweka mtego na kumnasa Sophia," alisema Kamanda na kuongeza
kuwa; "Siku ya pili Februari 18, mwaka huu asubuhi Sophia alikwenda
nyumbani kwa mama yake mdogo ambaye anaishi Mtaa wa Ruvuma na kumlaghai kuwa
kuna mtu alimwona Iringa na angependa kumwona ili aishi naye.
Mama yake mdogo alimwambia kuwa hajawahi kusafiri
kwenda mkoani Iringa na kukutana na mwanamume. Kamanda, Msikhela, alisema baada
ya Sophia kukwama kwa mbinu yake hiyo, alitumia uongo mwingine kwamba kuna
matajiri wanataka mtu wa kumwajiri, ndipo mama yake mdogo huyo alikubali.
Bila kujua kinachoendelea alikubali kupelekwa kwa mtu
aliyejifanya mnunuzi wa binadamu Mtaa wa Lizaboni. Alisema walipofika eneo la
tukio walimkuta mnunuzi akiwa tayari anamsubiri Sophia ili aweze kumkabidhi
huyo mama yake mdogo ili alipwe sh. milioni 6.5, bila ya kujua kwamba alikuwa
anaingia kwenye mtego wa Polisi.
Kamanda, Msikhela, alisema upelelezi wa tukio
unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazomkabili. Alisema wananchi waache kujihusisha na biashara ya binadamu
kwani ni makosa kisheria.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia,
Erick Bruno (30) kwa tuhuma za kumnyonga hadi kufa mpenzi wake, Daja Dungu (35)
wakati walipokuwa kwenye nyumba ya kulala wageni (jina tunalo) Manispaa ya
Morogoro.
Akizungumzia kutokea kwa tukio hlo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema tukio hilo lilitokea Februari 23, mwaka
huu saa 6.30 usiku katika karakana ya Kichangani ambapo mtuhumiwa alikodisha
chumba namba nane, akiwa na na mwanamke huyo.
“Februari 23, mwaka huu saa tisa na nusu mtuhumiwa
alifika kwenye nyumba hiyo akiwa ameambatana na huyo mwanamke kwa lengo la
kufanya ngono baada ya muda kukasikika kelele za kuomba msaada,” alisema Paulo.
Paulo alisema baada ya kelele hizo mlinzi wa nyumba
hiyo aliwaita watu na kumtaka mtuhumiwa afungue mlango, lakini alikataa kwa kudai
kuwa hakuna kitu kilichotokea, ndipo juhudi za kuufungua mlango zilifanyika na
kumkuta mwanamke huyo akiwa amefariki.
Aidha, Paulo alisema Polisi bado haijafanikiwa kupata
chanzo cha tukio hilo na kuwa upelelezi unafanyika ili mtuhumiwa aweze kufikishwa
mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Kamanda Paul, alisema mtuhumiwa anashikiliwa Polisi
kwa upelelezi zaidi na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment