Story Na Khamisuu Abdallah
Mwalimu madrasa ya Kadiria iliyopo
Amani mjini Zanzibar, Hamad Bakar Mohammed, anaetumikia kifungo cha miaka 15
jela kwa kosa la kumlawiti mwanafunzi
wake wa kiume, ameongezewa adhabu nyengine ya miaka 15 jela na Mahakama ya
Rufaa Tanzania.
Hukumu hiyo ilikuja baada
mshitakiwa huyo kupinga kifungo cha miaka 15 alichopewa na Mahakama Kuu
Zanzibar baada ya upande wa mashtaka kupinga uamuzi wa mahakama ya Mkoa Vuga,
kumuachia huru mshitakiwa.
Adhabu hiyo ilitolewa na Jaji
wa Mahakama Kuu Zanzibar,Abdul- hakim Ameir Issa.
Uamuzi wa kumuachia huru
mshitakiwa huyo katika mahakama ya Vuga, ulitolewa na Hakimu Makame Mshamba
Simgeni, baada ya kusema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka hautoshi
kumtia hatiani.
Jopo la majaji watatu akiwemo
Jaji Kimano, Jaji Njasiri na Jaji Luonda, walitupia mbali rufaa ya mshitakiwa
kupinga kifungo hicho na badala yake ikaamua kumuongezea kifungo chengine cha
miaka 15.
Adhabu hiyo mpya sasa inamfanya
mshitakiwa huyu kutumikia kiufungo cha miaka 30 jela.
Wakitoa hukumu majaji hao
walisema vitendo hivyo vimekithiri licha ya kukemewea na Serikali na kwamba
adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 13
mwaka huu huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Maulid Ame Mohammed kutoka
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
No comments:
Post a Comment