WATUMISHI wa serikali wilayani Masasi mkoani Mtwara,
wanaovaa nguo fupi yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania, maarufu
‘vimini’, wameonywa kuacha mara moja tabia hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego alitoa
maagizo hayo wakati akizungumza na watumishi wote wa wilaya ya Masasi, madiwani
na viongozi wa kimila wa kabila la Wamakua (Mamwenye).
Alisema tabia za baadhi ya vijana za kuvaa nguo
fupi, haikubaliki kwa jamii ya kitanzania. Alisema ni aibu na fedheha kwa
mtumishi wa umma, kuvaa nguo fupi kwa kuwa kitendo hicho kinakiuka maadili ya
utumishi wa umma.
Alisema kuna watumishi wengi tu wanavaa nguo
fupi kazini, hivyo amewaagiza maofisa rasilimali watu kushughulika na watu hao.
Dendego alisema anasikitishwa na vijana wa kiume, ambao wengi wao kwa sasa
wamekuwa wakivaa nguo zinazoonesha sehemu ya nguo zao za ndani kwa kushusha
chini suruali zao (mlegezo).
Alisema uvaaji huo haukubaliki na inabidi uachwe
na vijana wote nchini. Alisema vijana wengi wamekuwa wakiiga vitu vinavyofanywa
na wenzao wa mataifa ya Magharibi.
Aliwaonya kuwa si kila kitu kinachofanywa na
vijana hao ni cha maana na kinatakiwa kuigwa, badala yake waige masuala muhimu
na ya msingi katika maendeleo yao.
“Nyinyi vijana mliopo hapa ndani naomba
mnifikishie ujumbe wangu kwa wenzenu kuwa kuanzia leo yeyote atakayevaa nguo
fupi kwa wasichana na mlegezo kwa wavulana, atakamatwa na Jeshi la Polisi na
hatimaye kufikishwa mahakamani na sheria itachukua mkondo wake,” alisema
Dendego.
Dendego alisema vijana wavae mavazi ya heshima
wakiwa kazini na kwamba kuvaa kwao mavazi yanayokwenda kinyume na maadili ya
kitanzania, ni kujishushia heshima na hadhi yao kwa wazazi wao na
jamii.
Aliwaomba watumishi walio kazini kwa muda mrefu,
watoe maelekezo kwa vijana hao waachane na tabia zinazokwenda kinyume na
maadili ya utumishi wa umma.
Alisema kwa sasa kuna vijana wengi tu wanavaa
nguo fupi na zile zinazobana, hivyo kusababisha maumbile ya miili yao
kuonekana. Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment