“Kila kunapokucha naumiza kichwa
nifanye nini ili niweze kutengeneza pesa zitakazoniwezesha kuendesha maisha
yangu licha ya kuwa nimeolewa na kumkuta mume wangu tayari ana uwezo,” ndivyo
anavyosema Shamim Mwasha, mmiliki wa blogu maarufu ya 8020fashions.
“Pamoja ya kuwa nimeolewa na mtu ambaye uwezo wa kiuchumi sio mbaya lakini
hata siku moja sijawahi kupigia hesabu mali zake ndiyo maana naendelea
kujishughulisha.”
Shamim ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kufungua na kuendesha
blogu katika kipindi cha miaka tisa iliyopita hali iliyomuwezesha kujijengea umaarufu
mkubwa.
Anakiri kuwa wengi wamemfahamu kupitia blogu hiyo, lakini harakati zake za
kujikwamua kama mwanamke zilianza muda mrefu mara tu baada ya kuhitimu mafunzo
yake ya uandishi wa habari na kujiunga na Kampuni ya IPP.
“Nikiwa IPP ndipo ikaanzishwa tovuti ya darhotwire.com na kwa bahati
nikapata kazi kama mhariri wa habari.”
Shamim wenye watoto watatu anaeleza kuwa huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa
kujishughulisha na masuala ya mtandao.
Anasema wazo la kuanzisha 8020 alilipata baada ya kufungua duka la nguo
alipoona kuna umuhimu wa kufungua blogu ili kumuwezesha kutangaza bidhaa zake.
Anasema kuwa katika kipindi chote ameweza kuendesha maisha yake kwa
kutegemea blogu hiyo ambayo ina idadi kubwa ya watembeleaji na kupata matangazo
mengi ya biashara yanayomuingizia kipato.
Anaeleza kuwa licha ya wengi kumuona maarufu, anaishi maisha tofauti na
wanavyofikiria akiwa nje ya kazi yake. “Napata wakati mgumu kuona
wananichukulia mimi kama malaika, yaani wananiweka kwenye kundi la mastaa tena
mastaa wa Ulaya… Hapana sijafika huko mimi wa kawaida sana kuna wakati najuta
hata kwanini nilijitambulisha kama Shamim, bora watu wangeijua 8020 kuliko
ilivyo sasa. Naangaliwa kama mtu wa tabaka jingine, kitu ambacho siyo sahihi.”
Shamim anakiri kuwapo kwa migogoro na hali ya kutokuelewana kwa baadhi
wanawake wanaomiliki blogu hapa nchini na kueleza kuwa hilo linasababishwa kwa
kiasi kikubwa na chuki miongoni mwao na kutafuta attention. Anasema wengi
wanajikuta wakiingia kwenye migogoro kutokana na kukosa fikra mtambuka na
kushindwa kuwavutia wasomaji hali inayofanya kutafuta namna nyingine isiyo
rasmi.
No comments:
Post a Comment