WANAWAKE kama wazazi wametakiwa kutimiza
jukumu lao la malezi ya familia kwani wengi wao
kutokana na hali halisi ya maisha wameacha kufanya kazi hiyo na kuwaachia wadada wa kazi.
Mwito huo ulitolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete
wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri Kuu ya Tawi ya chama hicho, katika matawi ya Barabara ya Mchinga, Mitandi Magharibi na Kusini na Rutamba.
Mama Kikwete alisema kutokana na hali halisi ya
maisha, baadhi ya akinamama wana majukumu
mengi ya kazi na jukumu la malezi ya watoto
wamewaachia dada wa kazi, jambo ambalo sio zuri
kwa makuzi ya mtoto.
“Tunajua kutokana na hali halisi ya maisha,
wanawake wengi wanahangaika kufanya kazi ili
wapate fedha zitakazosaidia kuinua kipato cha familia, lakini hata kama una majukumu mengi jioni ikifika
jitahidi ukae na familia yako mle pamoja chakula cha jioni, kwa kufanya hivyo utajua matatizo
yanayowakabili. Imefikia hatua mama akimlisha
chakula mtoto wake aliyemzaa yeye mwenyewe
anakataa kula lakini akilishwa na dada wa kazi
anakula na akinamama wengine hata chai ya kunywa na mumewe anatengewa na dada wa kazi badilikeni jamani,” alisisitiza Mama Kikwete.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment