Mtoto wa takriban miaka miwili
kutoka eneo la Msisiri Mwananyamala jijini Dar es Salaam anayedaiwa
kuteswa na mama yake mzazi anapata matibabu katika hospitali ya
Mwananyamala kutokana na kile kilichotajwa na muuguzi wa wodi ya watoto
hospitalini hapo kuwa ni utapiamlo mkali na majeraha.
Vitendo vya utesaji dhidi ya mtoto huyo viligunduliwa na majirani ambao wamesema walikuwa wakishuhudia akipigwa na kufungiwa katika chumba ambacho inaishi familia yenye watoto watatu, jambo lililowasukuma kutoa taarifa polisi. BBC kutoka Dar es Salaam inaripoti.
Mwandishi wetu alipata nafasi ya kumuona mtoto huyo ambae anaonekana na majeraha mwilini hali inayoonyesha dhahiri mtoto Christina amepitia hali ngumu, kwani amejaa alama za kupigwa au kuchomwa na kitu chenye moto.
Pia suala la mtoto Christina kula vipande vya godoro lilisemwa na watu walioshudia tukio hilo sababu ikielezwa kuwa njaa kali kwa kuwa alikuwa akiachwa nyumbani peke yake kwa muda mrefu bila msaada.
Tukio hilo likanipeleka hadi eneo la Msisiri A Mwananyamala, huko nakutana na jirani na mama Christina, Abdul Moshi ananionyesha chumba cha mama huyo kikiwa kimefungwa kwa kufuli, kwanza anaelezea tukio hilo.
Kwa mujibu wa majirani mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote. BBC haikufanikiwa kumpata msemaji wa Polisi kuthibitisha hatua zaidi zilizochukuliwa dhidi ya mama wa mtoto huyo.
Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watoto mara nyingi vimeelezwa kutendwa na wasichana wa kazi au watu wengine baki, tukio la Uganda likiwa limetikisa vyombo vya habari. Lakini hili la mama mzazi kumtesa mtoto wake mwenyewe huenda likawa la utesaji na unyanyasaji wa aina yake.
No comments:
Post a Comment