Kama
unatafuta njia rahisi na haraka ya kuboresha sebule yako basi makala hii
inakuhusu. Utapata mawazo hapa ya kubadilisha muonekano wa sebule uwe bora
zaidi kwa haraka, bila gharama kubwa na bila wataalam.
Kwa
kuboresha muonekano wa ukuta suluhisho
la gharamna nafuu zaidi ni kupaka rangi. Paka rangi nyeupe au yoyote ya mwanga
kama unataka dari ionekane ndefu. Endapo hutapenda kupaka rangi basi bandika
karatasi za ukutani. Vinginevyo kama rangi ya ukuta inaonekana ni safi unaweza kuongeza muonekano kwenye kwa haraka na gharama nafuu kwa kutumia stika
za ukutani. Bandika stika kubwa na za rangi za giza kwenye maeneo unayotaka
kusisitiza au kwa kutengeneza boda kuzunguka kioo.
Stika za ukutani ni wazo
zuri za kubadilisha muonekano, pia ni gharama nafuu na unaweza kuziondoa pale
ambapo huzihitaji tena.
Funga
vioo ukutani kuongeza mwanga na nafasi sebuleni, vinageuza eneo dogo na lenye
mwanga hafifu kuonekana kubwa na lenye mwanga wa kutosha. Weka kioo ukuta
unaotazamana na dirisha ili kibebe mwanga unaongilia dirishani kiusambaze
chumbani. Pia kioo kikufungwa kutazamana na vitupio au maua yaonekane yapo
mawilimawili.
Sanaa zinabadilisha muonekano wa
chumba, tundika picha mpya za familia au fremu za michoro kuboresha muonekano
wa ukuta wa sebule yako. Picha na michoro hii unaweza kuviweka kwenye fremu za
rangi tofauti tofauti kuoongeza mvuto.
Sasa umemalizana na ukuta. Ukija
kwenye sofa ziboreshe pamoja na mito na kusheni zake kwa kushonea kitambaa
kipya. Ni gharama nafuu kuliko kununua sofa mpya, na vitambaa na mafundi wapo
wengi. Hata zile sofa zenye vitambaa ambavyo havivuliki ili kusafishwa kwa kina
vitakuwa vimeondolewa ama kufunikwa ndani ya hiki kipya. Kama una cherehani na
unaweza kushona foronya za mito na kusheni inakuwia nafuu sana kwani hata
kuzishona sio kazi kubwa.
Weka maua na miti artificial, hii inasaidia sana kuboresha
muonekano wa sebule. Pia baadhi ya maua na miti yanafanana kwa karibu sana na ya
asili kiasi kwamba kama hujaigusa ni ngumu kutofautisha. Pasipo shaka maua na
miti ni njia rahisi mno na ya gharama nafuu ya kuongeza rangi kwenye sebule
yako.
Ongeza mvuto kwa kubadilisha vikombe
vya taa za ukutani au vivuli vya taa za mezani. Pia kama taa ya ukutani ni
balbu pekee basi ivalishe kikombe. Na kwa gharama nafuu kama ulikuwa na hizi
taa za vivuli tayari, kwanini usibadili tu kivuli chake? Tembelea kwenye maduka
ya vitu vya sanaa wapo wanaouza vivuli vya taa kwa malighafi za asili kama
vitenge na mkeka.
Valisha upya madirisha ya sebuleni,
baada ya muda pazia huwa zinapauka hasa pale ambapo panapigwa na jua kali kwa
kipindi kirefu cha siku. Kusema la ukweli maduka yenye vitambaa vya mapazia au
mapazia yaliyoshonwa tayari ni mengi na yapo ya iana nyingi na kwa bei ya kuridhisha
ambapo walau kwa chini ya elfu 15 unapata pazia.
Sakafuni kama umetandika mazulia
makubwa ficha sehemu zinazoanza kuchakaa kwa vizulia vidogo badala ya kununua lingine
kubwa. Kumbuka hapa tunajuzana njia za gharama nafuu, kwa mfano kama umeweka
zulia la ukuta kwa ukuta, kuficha maeneo chakavu kwa vizulia vya kutupia ni
gharama nafuu kuliko kuondoa lote na kutandika jipya. Pindi utakapokuwa kwenye
hali nzuri kipesa ndipo utakaponunua kubwa jipya. Vizulia vya kutupia viwe na
rangi kali ili kuleta mvuto wa chumba. Rahisi zaidi - na haraka – kuliko kubadilisha
zulia zima!
Mpenzi msomaji, natumai umekubaliana
na mimi kuwa hizi ni njia za haraka zaidi na gharama nafuu za kubadilisha
muonekano wa sebule yako ili iwe na mvuto zaidi. Je kuna njia ambayo nimesahau?
Tuelimishane kupitia kwenye blogu yangu hapo chini.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi ambaye ana mapenzi na muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment