*Raia wachoma magari ya polisi, wapora silaha
*Wawafungulia mahabusu, wateketeza nyaraka
*Mmoja afariki, mabomu ya machozi yatumika
Jambo leo linaripoti kuwa MAPAMBANO makali yameibuka katika Kata ya Ilula mkoani hapa, kati ya
raia na polisi, hali iliyosababisha Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
kulazimika kutumia mabomu ya machozi kutuliza vurugu hizo zilizoibuka
kutokana na kifo chenye utata cha mwanamke mmoja.
Tukio hilo limetokea jana saa 5 asubuhi, ambapo vurugu hizo zilidumu
hadi saa 10 jioni, huku Kituo cha Polisi kikivunjwa, bunduki kuporwa na
nyingine kuchomwa moto na magari matatu na pikipiki moja ya polisi.
Wakielezea tukio hilo, wakazi wa Mji wa Ilula mkoani hapa, walidai
kuwa chanzo ni askari watatu watatu, akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi
cha Ilula kwenda kufanya msako wa wananchi wanaokunywa pombe muda wa
kazi.
Kutokana na msako huo, mwanamke huyo aliyepoteza maisha
aliyetambulika kwa jina la Mwanne Mtandi aliamua kukimbia kukwepa
kukamatwa na Polisi hao, kabla ya kukutwa nyuma ya jengo la klabu hicho
cha pombe za kienyeji kilichopo Mtaa wa Ilala mjini Ilula, akiwa
amekufa.
“Polisi hawa kila siku wamekuwa wakifika hapa klabuni na kukamata
watu, siku ya kwanza walimkamata marehemu na kumtoza faini ya sh. 20,000
na siku ya pili walimkamata yeye na mumewe na kuwatoza faini sh 40,000,
leo walikuwa wakija kumkamata tena na hapo ndipo mwanamke huyo aliamua
kutimua mbio, kabla ya kukutwa amekufa” alisema shuhuda wa tukio hilo,
Shida Ngwata.
Huku, Mkazi mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini,
alisema polisi hao walilazimika kutumia mabomu na risasi za moto
kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza, huku moja kati ya bomu
likiokotwa ambalo lilikuwa halijalipuliwa.
Alisema askari watatu ndiyo ambao walikuwa wakisakamwa na raia hao
ambao pia wamevunja vioo vya basi la Upendo kutokana na mkuu wa kituo
cha Ilula kukimbilia ndani ya basi hilo wakati akifukuzwa na raia hao.
Diwani wa Kata ya Nyalumbu, Ally Kikunga alisema kuwa, alipigiwa simu
na wananchi wake kujulishwa kuhusu vurugu hizo na baada ya kufika eneo
la tukio, alikuta mwanamke huyo akiwa mahututi, ila hakuweza kupata
msaada kutoka kwa wananchi wengine kumkimbiza hospitali .
Diwani huyo alilishauri jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu zaidi,
kwani alisema eneo hilo la klabu ni eneo ambalo wananchi wanapata
mahitaji mbalimbali na kwamba, mwanamke huyo alikuwa akifanya usafi
katika chumba chake cha biashara ya pombe.
Hata hivyo, alisema raia hao wameharibu mali mbalimbali na nyaraka
zote na kuwafungulia mahabusu wote waliokuwemo ndani, huku lori moja
lililokamatwa kituoni hapo likilindwa kuharibiwa kuwa halina kosa.
Vurugu hizo zilisababisha wasafiri wanaotumia barabara ya Kuu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kukwama kwa zaidi ya saa sita.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita pamoja na kamati ya
ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, ilifika eneo la tukio na kuthibitisha
kutokea kwa tukio hilo, huku akiahidi kutoa taarifa kamili ya mali
zilizoharibiwa na chanzo halisi cha tukio hilo, baada ya kukaa kikao na
viongozi wa jeshi la polisi na wale wa mji wa Ilula
Ingawa mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari mawili ya polisi
na pikipiki yakiwa yamechomwa moto, gari moja la askari pia lilichomwa
moto na magari mawili, moja la askari na daladala moja na basi la Upendo
kuharibiwa vibaya
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi,
alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, hakupatikana kwani alikuwa kwenye
kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, baada ya kikao hicho,
watatolewa taarfa kamili kuhusu vurugu hizo.
No comments:
Post a Comment