Monday, February 16, 2015

Nyumba zaidi ya milioni moja kupatiwa umeme jua.

Siku zinavyosonga ndivyo habari nzurinzuri kwa Watanzania zinavyochomoza, yaonekana mwaka huu mambo mazuri. Hili tembe nalo sijui litawekwa solar? Bado sana ila safari inaanza na hatua moja...tutafika tu.
Watanzania wengi wa vijijini hasa kanda ya kati wanaishi kwenye nyumba za tembe
TANZANIA imeingia katika mpango wa kutumia umeme jua ujulikanao kama One Milion Solar Homes, wenye lengo la kuzipatia nyumba milioni moja huduma ya umeme wa uhakika na salama kufikia 2017.
 Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Lutengano Mwakahesya alisema kuwa mradi huo utasaidia ajira kwa vijana.

Alisema kuwa mradi huo utatoa umeme kwa asilimia 10 ya watu nchini na pia kusaidia katika upatikanaji wa ajira 15,000 zinazohusiana na umeme wa jua.

Alisema kuwa kwa sasa asilimia 86 ya Watanzania, wanategemea mafuta ya taa na mishumaa kama njia kuu ya kujipatia mwanga hali ambayo haitoshelezi mahitaji husika.
Alisema kuwa kwa sasa mradi umeanza kufanya kazi kwa mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Geita ambapo gharama ya kujiunga ni Sh 15,000 na mtumiaji anaweza kununua umeme kama manunuzi ya umeme wa kawaida.

“Yani mteja anaweza kununua umeme huo wa jua na kuingiza namba za kiasi alichonunua katika mita ya umeme wa jua na kisha kupata umeme hasa kwa watu wa vijijini ambapo mradi huu unafanya kazi, na lengo ni kuhakikisha kuwa nchi inaongoza katika mradi wa nishati ifikapo mwaka 2030,” alisema Mwakahesya.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Off Grid Electric, Erica Mackey alisema mradi huo ambao umekuwa na mafanikio makubwa katika nchi nyingi hasa zinazoendelea, kwa hapa nchini utakuwa ukijulikana kama M-Power Off Grid na malipo kwa siku ni Sh 360.


Alisema kuwa kwa Tanzania, zimewekezwa zaidi ya bilioni 13 ambapo Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), limetoa dola bilioni tisa katika mradi wa kwanza wa kufikia nyumba zaidi ya laki moja.

No comments:

Post a Comment