Mkazi wa Loksale, Samweli Shani (47), akiwa amefungwa POP
baada ya kuvunjwa mikono yake na polisi, kushoto ni ndugu yake Gabriel Shani
akionyesha picha za X-ray alizopigwa zikionyesha jinsi mikono ilivyovunika.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, amekiri
kupokea malalamiko ya mkazi mmoja wa Loksale wilaya ya Monduli, Samwel Petro
Shani (47) ya kuvunjwa mikono yake miwili kutokana na kipigo cha askari Polisi
wa kituo cha Leskale.
Hata hivyo amesema kwamba kwa sasa yupo likizo ila
aliwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi Monduli (OCD) ili kupata undani wa
tukio hilo.
Imedaiwa kuwa kipigo hicho kimesababishwa na
mfanyabiashara mmoja ambaye alikodisha askari ili kumfunza adabu kwa kushindwa
kulipa fedha zake anazomdai zipatazo 250,000.
Hata hivyo mfanyabiashara huyo ambaye alijitambulisha kwa
jina la ,Shamimu alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi alikana kukodisha
askari wa kumpiga na kumvunja mkono mlalamikaji .
Alisema yeye kama mwananchi alienda kulalamika kituo cha
polisi kuhusu deni lake kwamba kilichotokea huko baada ya yeye kuondoka hafahamu.
Kwa mujibu wa maelezo ya mlalamikaji Samweli, askari hao hawakutaka kumkamata bali kuitoa
roho yake kwani walikuwa wakitumia chuma kinene kumpiga na kumvunja mikono yake
miwili huku mwingine alikuwa akimshambulia kwa rungu na mateke.
Alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februali 6,mwaka huu
majira ya saa 3 usiku na kwamba aliwatambua askari wawili waliomtesa kwa kipigo
kuwa ni Steven na Justini wote ni askari wa kituo hicho cha Loksale.
”Mnamo tarehe 6 mwezi huu majira ya saa 3 usiku,walikuja
askari wawili wakiwa wamevaa nguo za kiraia ,walinikuta nimekaa kwenye ukuta
nikiwa na kijana mmoja,walinikamata na kunifunga pingu wakiwa wamenikandamizia
chini ,walinipiga sana na kunivunja mikono yangu miwili”alisema Samweli
Akisimulia chanzo cha tukio hilo alisema, mfanyabishara Bi. Shamimu
alienda katika kituo hicho cha polisi na kuwaeleza askari hao kuwa alikuwa
akimdai shilingi 250,000 na kwamba sikuwa nimemlipa deni hilo.
”Ni kweli Shamimu alikuwa akinidai shilingi 250,000 ila
nilishamlipa shilingi laki moja na kubaki sh,150,000 ,hizo hela kuna msichana
nilimdhamini alikuwa mfanyakazi wa duka lake aliyedai alimwibia,ndipo mimi kwa
kuwa nilikuwa na mahusiano na msichana huyo nilikubali kulilipa deni hilo”alisema
Samweli
Alisema askari hao walimvamia na kumkaba kabari kisha
askari mmoja alimfunga pingu na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na rungu na
chuma na walipoona wamepoteza fahamu baada ya kumvunja mikono walimkokota hadi
kituo cha polisi na kuendelea kumpiga sehemu zingine za mwili ikiwemo miguuni.
”Baadae usiku wakiwa wamenifungia lokapu alikuja mkuu wa
kituo na kuniangalia ,alikuta hali yangu ni mbaya na kuondoka bila kusema
lolote”alisema.
Hata hivyo askari hao waliingiwa na woga kutokana na hali
yake na kuamua kumchukua usiku huo wa manane na kumpeleka katika kituo cha afya
kwa ajili ya matibabu.
Alieleza kuwa kesho yake askari hao walimchukua na
kumpeleka kituo cha polisi wilaya ya Monduli na kumweka lokapu.
Aliongeza kuwa mkuu wa upelelezi wa wilaya OC CID,aliyemtaja
kwa jina moja la Bw. Abichi alimfuata akiwa lokapu na kumwambia kuwa anataka
ampatie dhamana ila alitakiwa akubaliane na masharti ya dhamana .
”OC CID aliniambia kuwa nataka nikupatie dhamana ila
kwenye maelezo yako unatakiwa ueleze kuwa ulikuwa unatoroka ulinzi halali wa
polisi ukiwa na pingu ,na wakati ukikimbia ulianguka na pingu zikakuvunja
mikono yako ”alisema bw Shani.
Aliongeza kuwa hakukubaliana na kauli hiyo ndipo OC CID
alipoamua kumrudisha lokapu ,ambapo alikaa kwa muda wa siku nne wakimbembeleza
akubaliane na maelezo ya polisi .
Alisema kuwa aliamua kuwa na msimamo huo,hadi tarehe 12
walipoamua kumfikisha mahakama ya wilaya ambapo alisomewa shitaka , la kuvunja
na kuiba na kujaribu kutoroka polisi akiwa na pingu, suala ambalo ni uongo uliolenga
kupoteza haki yake ya kulalamikia jeshi hilo.
Imeandaliwa na Woinde Shiza wa libeneke la kaskazini blog
No comments:
Post a Comment