Kituo cha Televisheni cha Azam kimefanya mabadiliko
katika utangazaji wa taarifa za habari, huku kikimuajiri Jane Shirima kuwa
mkurugenzi wa televisheni.
Kuanzia jana taarifa ya habari ya Azam TV itakuwa ikisomwa
na watangazaji wawili na kutakuwa na pea tatu tofauti za watangazaji.
Naibu Mtendaji Mkuu wa Azam Televisheni, Tido Mhando
alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wamejiandaa vilivyo kuhakikisha kuwa
mbali na studio bora wanakuwa pia na kikosi cha wanahabari wenye uwezo mkubwa.
“Hapana shaka tunao vijana wazuri sana, lakini pia
tulihitaji waandishi wenye uwezo na ujuzi wa hali ya juu ili kuendana na
mikakati, fikara na mipango yetu ya kufanya mageuzi makubwa ya hali ya
utangazaji wa habari za televisheni nchini,” alisema Tido.
“Duniani pote vituo vingi vya televisheni na redio
vilianzishwa kwa mtindo kama huu. Kituo cha lugha ya Kiingereza cha Al Jazeera
kilipoanzishwa kiliajiri watangazaji waliobobea kutoka mashirika kadhaa makubwa
ya utangazaji duniani ikiwa ni pamoja na CNN, BBC na NBC. Lakini pia lazima
kuwepo na hadhi ya kuweza kuwavutia watu hao,” alisema mkurugenzi huyo wa
zamani wa redio Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Tido aliwataja baadhi ya waandishi na watangazaji ambao
wameungana na Azam TV kuwa ni Charles Hilary, Baruani Muhuza, Ivona Kamuntu na
Fatuma Almasi Nyangasa.
“Watangazaji hao sasa wataungana na wasomaji wetu wazuri
wa siku nyingi Rehema Salum na Nurdin Suleiman kukamilisha pea tatu za wasomaji
wa mtindo wa wawili wawili,” alifafanua Tido.
Tido alisema leo na kesho habari itasomwa na Charles
Hillary na Ivona Kamuntu wakati siku mbili nyingine itakuwa ni zamu ya Baruhani
Muhuza na Fatuma Nyangasa huku Rehema Salum na Nurdin Suleiman nao wakiwa na
zamu yao.
Alisema licha ya taarifa ya habari ya saa mbili usiku pia
wanatarajia hivi karibuni kuanzisha taarifa ya habari ya saa saba mchana
itakayokuwa ikiendeshwa na Zainab Chondo na Raymond Nyamwihula.
“Mpango wote huu wa mabadiliko haya ya utangazaji na
upatikanaji wa habari wa Azam TV utakuwa unasimamiwa na kuratibiwa na Joseph
Warungu aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza kitengo cha BBC cha Focus on
Africa,” alisema Tido.
Tido aliwataja wanahabari wengine mbao wamejiunga na Azam
TV kuwa ni Taji Liundi, Phillip Cyprian, Mwanga Kirahi na Jane Shirima ambaye
ataanza kazi leo kama mkurugenzi wa televisheni.
Wakati huohuo, Tido alisema kuanzia Jumamosi wiki hii
watazindua kipindi maalumu cha mahojiano ya kina kwa wote waliotangaza na
kuchukua fomu za kugombea nafasi ya urais. Kipindi hicho kinachojulikana kwa
jina la Funguka kitakuwa kinatangazwa kila siku kuanzia saa moja kamili usiku.
Tido alisema katika muda
wa mwezi mmoja ujao Radio ya Azam Media Group itakayojulikana kwa jina la UFM
itakuwa hewani.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment