Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya mauaji
ya kukusudia iliyokuwa ikimkabili mfanyabiashara Marijan Abubakar, maarufu kama
Papa Msofe (50) na mwenzake, Makongoro Joseph.
Hakimu Mkazi, Renatus Rutta aliifuta kesi hiyo chini ya
kifungu cha 91 (1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Aliifuta baada ya Wakili wa Serikali Wankyo Simon, kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kuonyesha kuwa hana nia ya
kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Msofe na Makongoro wamesota rumande kwa takriban
mwaka mmoja sasa kutokana na kile kinachelezwa ni upelelezi kusubiriwa ukamilike.
Msofe kwa mara ya kwanza alifikishwa kortini Agosti 2012.
Hata hivyo baada ya kuachiwa huru Makongoro aliruhusiwa
huku Msofe akifunguliwa kesi nyingine ya kughushi.
Katika kesi hiyo mpya, Msofe anadaiwa kuwa Desemba 23,
2004 katika Wilaya ya Ilala kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka ya
kuhamisha haki ya umiliki wa nyumba namba 288 ambayo ni mali ya mfanyabiashara
wa madini Onesphory Kituli (kwa sasa marehemu).
Ilidaiwa kuwa Msofe kwa nia ya kudanganya alighushi
nyaraka hiyo akionyesha Desemba 13,2004, Kituli alihamisha haki yake ya umiliki
wa nyumba hiyo kwake wakati akijua ni uongo.
Mbali na shtaka hilo, Msofe anadaiwa kuwa kati ya Desemba
23,2004 na Machi 30, 2005 akiwa na nia ya kidanganya alitoa nyaraka hizo za
uongo kwa Kamishna wa Ardhi kwa lengo la kuhamisha umiliki kutoka kwa Kituli
kwenda kwake.
Upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa upelelezi
wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 9, 2015 na ametakiwa kuwa na
wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 10 milioni.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment