Matukio ya Watanzania kukamatwa nje ya nchi wakiwa na
dawa za kulevya zilizopigwa marufuku yanazidi kukithiri baada ya mwanamke mmoja
kukamatwa na kilo 74 za dawa aina ya ephedrine kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mumbai, India.
Mwanamke huyo, Chambo Fatuma Basil alikamatwa na Kikosi
cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha India kilichopata taarifa za kuwapo kwa
mtu huyo ambaye alikutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.
Kwa mujibu wa tovuti ya hindustantimes.com limewanukuu
maofisa wa Idara ya Uhamiaji wa India, Kitengo cha Intelijensia cha Uwanja wa
Ndege (AIU) wakisema Chambo alithibitishwa Mtanzania baada ya kufanyia ukaguzi
na kukibainisha kuwa kiwango alichokutwa nacho ni kikubwa kulivyo mzigo wowote
wa dawa za kulevya uliowahi kukamatwa kwenye uwanja huo wa ndege.
Maofisa hao walisema walimnasa mwanamke huyo baada ya
kudokezwa na kufuatilia taarifa ya abiri huyo aliyekuwa akielekea Dar es Salaam
kupitia Doha, Qatar.
“Mtuhumiwa alikamatwa saa 7:00 mchana. Mbwa maalum
alielekezwa kukagua mizigo yake iliyokuwa inaingizwa chini ya ndege na akatoa
ishara chanya,” alisema Milind Lanjewar, kamishna wa ziada wa ushuru wa Uwanja
wa Ndege.
Mizigo yake mitatu ilikuwa imewekwa pakiti za unga mweupe
unaosadikiwa kuwa wa methaqualone au mandrax, dawa ambayo hutumiwa kama mbadala
wa cocaine, imeandika tovuti hiyo.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Madawa ya Kulevya
nchini, Godfrey Nzowa alisema kwa kuwa mwanamke huyo amekamatwa nchini India,
Tanzania haiwezi kuingilia kwa undani ingawa wanasubiri iwapo India watawapigia
simu.
“Kila nchi ina sheria yake na ina uwezo wa kumchukulia
hatua Fatuma kwa kuwa yupo ndani ya nchi hiyo,”alisema.
Nzowa alisema nchi nyingi duniani zipo kwenye vita dhidi
ya dawa za kulevya hivyo hashangai kwa Mtanzania huyo kukamatwa nchini India.
Nzowa alisema dawa hizo ni kemikali au vibashirifu
vinavyotumika kutengeneza dawa za kulevya na huzalishwa zaidi India.
Alisema ephedrine zinatumika kutengenezea dawa za
kikohozi lakini kinachojitokeza watu wanabadilisha matumizi yake na kutengeneza
dawa za kulevya.
Nzowa alisema aina hiyo ya vibashirifu inalimwa kihalali
nchini India kwa vibali maalumu kwa ajili ya kutengenezea dawa ya kikohozi .
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment