Serikali ilianzisha mpango wa kujenga shule za sekondari
za kata moja ya mikakati ikiwa kupunguza adha ya umbali kwa wanafunzi na
kusogeza huduma za elimu jirani na wananchi ili kila mtoto apate haki ya kupata
elimu.
Pamoja na mpango huo kutekelezwa kwa asilimia kubwa, bado
adha ya umbali wa shule kwa baadhi ya wanafunzi iko palepale, hali
inayosababisha wanafunzi wengi kuacha masomo.
Shule ya Sekondari Shantamine katika Kata ya Mtakuja,
Geita mjini ni miongoni mwa shule nyingi mkoani Geita na maeneo mengi
nchini ambayo bado wanafunzi wana changamoto ya umbali wa kuifuata elimu
au kurudi nyumbani.
Zaidi ya wanafunzi 27 wameacha masomo kwenye shule hiyo
katika kipindi cha miezi mitano tangu kuanza kwa mwaka huu.
Taarifa zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 200 walioanza
kidato cha kwanza katika shule hiyo, waliomaliza kidato cha nne mwaka
jana ni wanafunzi 50.
Takwimu hizo zinamaanisha kwamba wanafunzi 150 waliacha
shule huku sababu kubwa ikiainishwa kuwa ni umbali, pia mimba kwa wasichana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Elimu wa Mkoa wa Geita,
Eufransia Buchuma aliyoitoa mwaka 2013, wanafunzi 8,606 sawa na asilimia 50.2
kwa katika Mkoa wa Geita hawakumaliza kidato cha nne mwaka huo kati ya
wanafunzi 17,113 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2010.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Kakila Swillah
anabainisha kwamba tatizo hilo ni kubwa katika shule yake akieleza kuwa
limesababisha wanafuzi wawili kuandika barua ya kuomba kuacha shule mwanzoni
mwa mwezi Mei mwaka huu.
“Hii inaonyesha ni jinsi gani tatizo hilo ni kubwa.
Nimekuwa mwalimu mkuu katika shule nyingi, lakini sijawahi kuona mwananfunzi
kwa hiari yake mwenyewe anaomba kuacha masomo kwa kigezo cha umbali. Hili ni
tatizo,”anasema mwalimu huyo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment