Friday, June 12, 2015

Nusu saa kabla wageni hawajafika nyumbani kwako: Ni wapi pa kusafisha?

Katika makala ya leo tunataka kuangalia ni namna gani ya kuandaa nyumba pale wageni wanapotarajiwa kufika muda mchache ujao. Watanzania tunapenda na ni wakarimu kwa wageni kwa hivyo hapana shaka kuwa wengi wetu tunajiandaa kwa mambo kadha wa kadha tunapotegemea wageni nyumbani.

Hivyo basi katika kufanikisha
makala hii nilimtembelea rafiki yangu Esther nyumbani kwake kuona yeye na familia yake wanajiandaaje kwa ugeni nusu saa kabla haujawasili. Esther akanikaribisha mlo wa mchana na familia yake na baada ya kula familia ilianza kusafisha. Ndipo nikamuuliza hili swali yeye na watoto wake: Kama wageni wanafika ndani ya nusu saa na ndani ya nyumba mazingira hayajakaa sawa, ni wapi ambapo mtasafisha kwanza? Ni swali rahisi, na ukweli kuwa sio mara ya kwanza kupata wageni, lakini nilishangaa kwa jibu la kila mmoja kwa ajili wote tuna majibu tofauti ya orodha ya maeneo ya kuanza kusafisha ili kuweka nyumba nadhifu kabla wageni hawajaingia nyumbani nusu saa kabla!

Ukweli ni kwamba majibu yanategemea pia na mambo mengine – je hawa wageni ni wa kulala? Wanapita tu ama wanategema kukaa muda na kuandaliwa chakula? Kwa hivyo swala langu likalenga kuwa wageni hao ni mara ya kwanza kuja nyumbani na wanapita tu kwa muda mchache ambao sio muda wa chakula. Na ni wageni wako wa karibu sana na wangependa kuona mahali unapoishi. Na kwa vile ni watu wako wa karibu na hawajawahi kufika kwako bila shaka itakupasa kuwatembeza  maeneo mbalimbali ya nyumba yako. Una nusu saa ya kusafisha. Ni wapi pa kuzingatia? Soma majibu hapa ambapo nawe msomaji wangu bila shaka utakuwa umejifunza kitu.

Esther na familia yake wananiambia kwanza atahakikisha vyombo vyote jikoni ni visafi na sinki halina chombo kichafu, atafuta kaunta za jiko na kuweka mpangilio. Anasema anadhani hakuna anayependa kuona mabaki ya chakula hadharani.

Baada ya hapo ataenda sebuleni na kuondoa mrundikano wowote utakaokuwepo kama vile kazi za watoto za shuleni kwenye meza ya chakula au ya kahawa, magazeti na vitabu. Pia atafuta meza na vimeza vumbi. Halafu atapanga mito na vitambaa vyovyote vya makochi na meza vizuri wakati chochote kichafu atakiweka kwenye kapu la nguo za kufua. Hapo tukumbuke kuwa ana nusu saa tu wageni waingie.

Halafu ataelekea bafuni, hasa lile ambalo linaweza kutumiwa na hao wageni na kuweka mazingira safi kwa dakika mbili. Atahakikisha kuwa bafuni kuna taulo kavu na safi la kufutia mikono , kuna karatasi za chooni na bakuli la choo pamoja na sinki ni visafi.

Halafu atatoka kwenye varanda na ujia. Je kila kitu kinavutia, njia iko wazi na ni safi?

Muda uliobakia atautumia kupitisha ufagio sakafuni na kukung’uta tandiko la mlangoni.
Wakati huohuo akiwaekeleza watoto waende vyumbani kutandika vitanda vyao na kuweka nguo chafu kwenye makapu.

Esther anasema chumba cha watoto cha kuchezea hatakigusa kwa ajili ni cha michezo kitatakiwa kubaki hivyohivyo kuonyesha kuwa kuna michezo inaendela huko.

“Ndani ya hizo dakika thelathini nitakuwa nimemaliza na nitajiamini kuwa nyumba iko vizuri kwa ugeni,” anasema Esther.

Baada ya majibu ya rafiki yangu Esther, msomaji wangu utakuwa umejifunza kwamba haitakiwi kuchukua siku nzima kuweka mandhari ya nyumba nadhifu. Hata dakika thelathini zinaweza kufanya tofauti kubwa!

Sasa ni wakati wako. Ningependa kujua unawezaje kuifanya nyumba yako nadhifu ndani ya nusu saa? Nyumba tunazoishi zinatofautiana japo mahitaji ya msingi ni yaleyale, je orodha yako ni sawa na ya Esther? Unajua ni wapi utaanza kupaweka sawa? Au labda wewe ni kati ya wale waliobahatika kuwa na nyumba nadhifu masaa 24 kwahivyo hupaswi kujilinganisha na hali hii? 

Au hata kama mazingira ya nyumba yako hayajakaa vizuri ni sawa tu mgeni kuingia. Ningependa kusikia kutoka kwako!


Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment