BARAZA la Wazee wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), linatarajia kukutana kesho jijini Dar es Salaam ili
kuanza kujadili mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM.
Hadi kufikia jana, wagombea waliochukua fomu za kuomba kugombea nafasi ya urais
ndani ya CCM wamefikia 39.Mwenyekiti wa baraza hilo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake ni Bw. Pius Msekwa ambapo dhamira ya kukutana huko ni kuanza kupitia mambo mbalimbali ili kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata mjini Dodoma jana ambazo zimethibitishwa na mmoja wa Maofisa wa CCM Makao Makuu, zinasema baraza hilo linaundwa na marais wote wastaafu akiwemo Amani Abeid Karume, Benjamin Mkapa pamoja na Makamu wa Rais wastaafu.
"Ni kweli Jumatano (kesho), Baraza la Wazee litakutana Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Mzee Mwinyi, Katibu Mzee
Msekwa likijadili mchakato wa kumpata mgombea urais CCM.
"Muda umekaribia na baadhi ya vikao vya kamati vimeanza," alisema ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa sababu yeye si msemaji wa chama.
Alisema Ukumbi wa White House, uliopo mjini Dodoma, utaanza kutumika baada ya kupatikana wagombea watano ambao watachujwa na kubaki watatu na hatimaye kumpata mmoja ambaye atapatikana katika ukumbi mpya uliopo nje kidogo ya mji huo.
Wakati baraza hilo likutana kesho, tayari Kamati ya Ilani ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Stephen Wassira, imeanza kukutana ili kuandaa na kukamilisha ilani ya mpya ambayo wagombea wengi wanaisubiri ili waweze kuitumia.
Mji wa Dodoma kwa sasa umekuwa na hekaheka nyingi ambazo zinaendelea kufanywa na wapambe wa wagombea wa nafasi ya urais na ulinzi umeimarishwa katika maeneo mbalimbali.
Mgombea mwingine ajitokeza
Wakati masikio ya Watanzania yakielekezwa mjini Dodoma katika kipindi cha lalasalama ambacho baadhi ya wagombea urais wameanza kurudisha fomu wakisubiri kujadiliwa, jana mwanachama mwingine wa CCM amechukua fomu na kuwa mgombea wa 39.
Mwanachama huyo ni Rita Ngowi ambaye ni mwanamke akisema anataka kuhakikisha anainua maisha ya Watanzania kiuchumi ili waweze kuwa na maisha mazuri.
Alisema kama CCM kitamteua kuwa mgombea urais na kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, atahakikisha watu wote wakiwemo vijana ambao hawana uwezo, wanawekwa sehemu moja waweze kusaidiwa na wengine kutafutiwa kazi za kufanya ili wajiingizie kipato.
Aliongeza kuwa, wazee wote ambao ni wastaafu atahakikisha wanakuwa na maisha mazuri tofauti na sasa na kuendeleza mazuri yote ambayo yataachwa na Rais Kikwete.
"Nitahakikisha kunakuwa na kituo cha wastaafu na wasiojiweza ili waweze kusaidiwa na vyanzo vyote vya mapato ya Serikali nitavidhibiti ili kuondoa tatizo la rushwa," alisema.
Wagombea warudisha fomu
Baadhi ya wagombea waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, jana wameendelea kurudisha fomu akiwemo Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw.Stephen Wassira.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Dkt. Magufuli alisema amefika mikoa 23 na kupata wadhamini ili kutekeleza matakwa
ya chama chake ya kutafuta wadhamini 450.
"Nilichukua fomu Juni 4, mwaka huu, nimefika mikoa 23 na kupata wadhamini," alisema Dkt. Magufuli ambaye aliwasili katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM saa mbili asubuhi na kukabidhi saa nne asubuhi akiwa na gari aina ya Marcedes Benz lenye namba za usajili T 642 AFB.
Wassira azungumza
Kwa upande wake, Bw. Wassira ambaye alichukua fomu Juni 3, mwaka huu, aliwaomba Watanzania wamwombee ili achaguliwe katika tano bora, tatu bora na hatimaye awe mgombea mteule ambaye atakipa chama hicho ushindi wa kishindo.
Alisema wanaojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wanamtambua vizuri kwani wakati wanaandamana baada ya Uchaguzi Mkuu, yeye atakuwa anakwenda Ikulu
MAJIRA
No comments:
Post a Comment