MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa
ya Binadamu Dk Mwele Malecela mtoto wa Makamu wa zamani wa CCM John Malecela ni
miongoni mwa wana CCM ambao wamejitosa kugombea urais kupitia CCM.
Dk Mwele katika maisha
yake mengi kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa mtumishi katika Taasisi ya Taifa ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambako alianza kazi akiwa kijana na
akapanda hadi kuwa mtafiti mkuu na baadaye akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Licha ya kukulia
katika familia ya mwanasiasa maarufu nchini, lakini Dk Mwele hajawahi
kujitokeza hadharani kushiriki kwenye masuala ya siasa. Kama akichukua fomu
hiyo kesho, atakuwa ni mwanamke wa pili kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais
kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Mwanamke mwingine ni
Balozi Amina Salum Ali wa Zanzibar. Jana Waziri wa Malisili na Utalii, Lazaro
Nyalandu na wanachama wengine wawili wa CCM walichukua fomu za kuwania urais.
Nyalandu alikuwa wa kwanza kufika katika ofisi za CCM kuchukua fomu akiwa
amefuatana na familia yake na wafuasi wake kadhaa.
Baadaye alifuatiwa
na mwanachama mwingine wa CCM, Peter Nyalali, ambaye ni Ofisa mstaafu wa Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kufuatiwa na mwanachama wa chama hicho kutoka
wilaya ya Muleba, Leonce Mulenda.
Akizungumza mara
baada ya kuchukua fomu, Nyalandu alisema hatua hiyo ni ishara ya yeye kuanza
safari ya ndoto yake ya kuchukua majukumu ya urais kwa lengo la maendeleo ya
nchi hii chini ya misingi aliyoianzisha Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius
Nyerere.
Kwa upande wa
Nyalali, alisema atalenga katika kuimarisha uchumi kwa kuzingatia Katiba ya
nchi na ya chama na kuleta mabadiliko chanya ndani ya CCM na kwa Watanzania
ambao wamekuwa hawanufaiki na fursa zilizopo nchini.
Kwa upande wa Leonce
Mulenda, alisema atahakikisha Katiba ya Chama na maamuzi yanatekelezwa kama
inavyotakiwa na kuwa chama imara kitakachosaidia serikali isiwe legelege.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment