Wote tunathamini usingizi mwororo, lakini ni vigumu kuupata
kama matandiko ni machafu. Ndipo inaleta maana kuwa matandiko yanapaswa
kusafishwa mara kwa mara kadri ya matumizi.
Kutokufua
matandiko yako mara kwa mara kutachangia kuongezeka kwa matatizo ya kiafya kama
mzio na pumu. Kama wewe, mwenzi wako au mtoto anaumwa, hakikisha unafua shuka
kila siku na kuabadilisha foronya kila siku ambazo mgonjwa analalia.
Wengi
wanatumia foronya kuvalisha mito yao, kama unatumia foronya sanasana unatakiwa
kufua mito yako mara moja ndani ya miezi miwili, wakati foronya inabidi
zifuliwe kila wiki. Mafuta na uchafu kutoka kwenye nywele zetu unaweza kuzama
ndani hadi kwenye sponji zilizotengenezea mto. Kufua foronya kutazifanya ziwe
safi na kuondokana na harufu mbaya.
Kuhusu
muda shuka zinapotakiwa kufuliwa baada ya kutumika kunategemea zaidi na chaguo
la mtu. Wapo wanaopenda kufua angalau kila wiki na wapo wanaofua japo kila
baada ya wiki mbili. Na hii inategemea pia na mazingira yalipo nyumba, kuna
nyumba ambazo vumbi kufika chumbani ni rahisi sana na zipo ambazo vumbi
halifiki chumbani. Ni vizuri kuwa na hisia kuwa shuka unazolalia ni safi na
kuwa na kitanda kilichotandikwa shuka safi.
Shuka
zinapata uchafu na mafuta kutoka kwenye miili yetu na pia udongo ambao unaweza kusababisha
madoa. Hakikisha unacheki na kuondoa madoa kila mara unapozifua. Pia epuka
kufua shuka na maji ya moto kwani maji ya moto yatazifanya zisinyae. Unaweza
usigundue kusinyaa huko hadi pale unapozirudisha tena kitandani kwa ajili ya
kutandika. Maji ya uvuguvugu ni mazuri zaidi kufanya shuka ziwe safi bila
kusinyaa.
Kuamua
ni kwa kila muda gani kufua blanketi zako inategemea na matumizi. Kama una
blanketi mwishoni mwa kitanda ambalo halifunguliwi likatumika, kulifua kila baada
ya miezi michache italeta maana. Ila kama blanketi linatumika kila siku au kila
usiku unaweza kuhitajika kuliweka kwenye ratiba ya kulifua kila baada ya wiki
mbili. Kuwa makini kufuata maelezo ya utunzaji wake kwenye lebo na fua kuendana
na muongozo. Kama blanketi halitumiki sana kuwa makini na uchujaji rangi, kama
una wasiwasi ni vyema kufua blanketi peke yake bila kuchanganya na nguo
nyingine.
Endapo
una komfota au duveti ambalo linatumika tu kama pambo la kitanda ukiwa
umeshakitandika kukifanya kionekane kunyooka vizuri, kama hamna chochote kilichomwagikia,
huna haja ya kuyafua zaidi ya mara mbili kwa mwaka. Kwa ajili kwa kawaida haya
ni makubwa ni vyema yafuliwe kwenye mashine za kufulia. Endapo huna mashine
hiyo basi peleka kwa dry cleaner.
Kwa
upande wa godoro, kutumia foronya la godoro ni njia nzuri ya kuongeza maisha ya
godoro lako. Foronya hizi zinazilinda godoro lililoko ndani yake na zinatakiwa
kuondolewa na kufuliwa japo mara mbili kwa mwezi. Na pia endapo kuna chochote
kimemwagikia ni vyema kuvua foronya na kusafisha doa hadi kwenye godoro kwa
kusponji eneo la doa.
Yale
matandiko ya ziada kwa ajili ya kupambia kitanda kwa ujumla huwa hayatumiki na
kwa maana hiyo hayachafuki mara kwa mara. Kama wewe ni mtu mwenye mzio na vumbi
unaweza kuyafua mara moja ndani ya miezi miwili au mitatu. Kwa watu wengine wote
yafue mara mbili tu kwa mwaka inatosha.
Kumbuka kuwa matandiko ni yako unayalalia
wewe mwenyewe kwahivyo kuyaweka katika hali ya usafi kila wakati ni kwa faida
yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea
www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment