Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Benard Membe, amekana kuwa na undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe (62) ambaye
Juni 8 mwaka huu alitangaza nia ya
kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM) na kisha jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti hicho,
alisema ingawa amekuwa akifananishwa na Rais Kikwete mara kadhaa; hakuna
ushahidi wowote wa kibailojia unaothibitisha kwamba wana uhusiano wa kindugu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kuchukuwa fomu hiyo kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma jana, Membe alisema
baadhi ya watu wamekuwa wakimfananisha na Rais Kikwete lakini hawana undugu
wowote baina yao.
“Kungekuwa na aibu gani au hasara gani kuficha kwamba
mimi ni ndugu wa damu wa Rais Jakaya Kikwete. Mimi siyo ndugu wa mheshimiwa
Rais, lakini binadamu tunafanana…rangi yangu, sura yangu na ufupi wangu
nimeuchukua kwa mama yangu,” alisema Membe na kuongeza:
”Aliyekuwa Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika (sasa
marehemu) wakati fulani pia aliwahi kunifananisha na Rais Kikwete. Naomba
nitamke wazi kwamba sina undugu wa damu na mheshimiwa Rais.”
Alisema hali hiyo pia iliwahi kumkuta baada ya Wamarekani
weusi (Afro Americans) kumkaribisha Marekani wengi walimuomba kupiga naye picha
wakidhani ni Rais Kikwete lakini baadaye aliwaeleza ukweli kwamba yeye hakuwa
Rais Kikwete.
Hadi kufikia jana mchana makada wa CCM waliotangaza nia
ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama
hicho na kisha kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania kiti hicho walifikia
20.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment