Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete anayesoma shule ya kimataifa
ya Feza, Khalfan Jakaya Kikwete (17) ameiwakilisha vema Tanzania katika
shindano la kusaka wanafunzi wenye akili nyingi 'Genius Olympiad' lililofanyika
Oswego, Marekani mwaka huu.
Kwa mujibu wa mtandao wa www.geniusolympiad.org,
mwaka huu nchi 69 zilishiriki kwa kupeleka kazi 1,171. Kazi 401 zilikidhi
vigezo na kupokewa. Shule za kimataifa za Feza ziliwasilisha kazi nne na
kushinda medali moja ya dhahabu na tatu za shaba.
Kazi iliyoshinda medali ya dhahabu iliitwa
'Vcardin' iliyoandaliwa na kuwasilishwa na Khalfan na Seif Yahya Mhata ambao
wote ni wanafunzi wa shule za Feza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Khalfan alisema kazi yao imelenga
kurahisisha mawasiliano ya kimataifa kwa kuwa na njia ya uhakika ya
kuwasiliana.
"Mradi huu unahusu kubadilishana kadi za mawasiliano
kwa njia ya mtandao. Ni muhimu sana kwa mawasiliano hasa ya wafanya biashara,
lakini inahitaji uwe na simu ya kisasa yenye intaneti au kifaa kingine chenye
intaneti," alisema Khalfan aliyekuwa amefuatana na Mhata.
Kazi nyingine kutoka Feza zilizoshinda medali za shaba ni
'The Fault of Humanity' iliyoandaliwa na Prince Mwemezi ambaye alipiga picha ya
moto ukiunguza miti eneo la Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam na
kuonyesha athari za mazingira zitokanazo na uchomaji misitu.
Medali nyingine ya shaba imeletwa katika shule ya Feza na
wanafunzi wawili Goodluck Komba na Sajjad El-Amin ambao walianza kazi
inayoonyesha namna mkaa unavyoweza kupatikana kupitia karatasi na takataka
badala ya kukata miti.
Veronica Ndomba, mhitimu wa kidato cha sita mwaka
huu katika shule ya Feza Girls, aliandaa kazi ya kuzuia uchafuzi wa mazingira
ya bahari kwa kuelimisha watu kuhusu kutotupa taka, mafuta na uvuvi haramu
baharini na kushinda medali ya tatu ya shaba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment