Aisha, katikati nyuma akiwa na wanae watatu shuleni |
“TANGU nilipozaliwa mkoani Morogoro mwaka 1990, sikupata
nafasi ya kujiunga na masomo maana familia yetu ilikuwa ya kuhama hama na baba
hakuonesha nia ya kunisomesha kabisa.”
Ndivyo anavyoanza
kusema Aisha Ally (25), mama mwenye mume na watoto watatu ambao anasoma nao
katika Shule ya Msingi ya Meru, jijini Arusha.
Mama huyo anasoma
darasa la tano huku mwanawe Philomena (9) akisoma darasa la nne, Giftgod (5)
akiwa darasa la kwanza pamoja na Thecla (3) ambaye yuko shule ya awali hapo
hapo katika Shule ya Msingi Meru.
Kisa, huruma Aisha
aliyezungumza na gazeti hili wiki hii, amesema matatizo yaliyoikumba familia
yao huko nyuma, yalichangia ashindwe kabisa kuhudhuria masomo na badala yake
akajikuta akiolewa na kupata watoto.
Kwa mujibu wa Aisha,
alipanga kuanza darasa la kwanza kabisa, lakini walimu wa Shule ya Msingi Meru
walimshauri aanzie darasa la nne kwani umri wake ulikuwa mkubwa.
Sababu nyingine
iliyosukuma walimu watoe ushauri huo kwa mujibu wa Aisha, ni binti yake mkubwa,
Philomena ambaye wakati huo alikuwa darasa la tatu na hivyo kama angeanza
darasa la kwanza, angekuwa amemzidi mama yake kwa darasa moja.
Viboko
Akizungumza kwa
kujiamini, Aisha alisema umbo lake dogo na ufupi wa kimo, vimemsaidia kuonekana
kama mwanafunzi wa kawaida kiasi kwamba baadhi ya walimu wasiojua historia yake
na wageni, humchukulia kama wanafunzi wengine tu na kumchapa viboko pale
anapokosea.
Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Meru, Mussa Luambo amesema kuna utaratibu maalumu wa kusaidia
wanafunzi waishio kwenye mazingira magumu, wakiwemo wale waliokosa elimu
utotoni.
Kwa mujibu wa
Mwalimu Luambo, Aisha ni miongoni mwa wanafunzi 20 walio kwenye kitengo hicho
na baadhi ya walimu wameamua kuchangia fedha kutoka mifukoni mwao ili
kuwasaidia.
“Kwa kweli wanafunzi
wenye umri mkubwa huwa hatuwachapi kabisa ila tu kwa upande wa Aisha mwili wake
mdogo huwa unamponza. Kuna walimu wasiomfahamu hivyo hudhani ni mwanafunzi wa
kawaida,” alisema Mwalimu Luambo.
Mtoto ashuhudia
Akizungumza na
gazeti hili, binti mkubwa wa Aisha, Philomena alisema; “Wakati mwingine huwa
tunachapwa viboko pamoja na maumivu yakizidi mimi na wanafunzi wengine hulia
machozi, lakini mama huwa halii kama sisi, tena haogopi wala haoneshi kujali
kupewa adhabu.”
Hata hivyo, Aisha
anakiri kuwa viboko ndio suala linalomkera zaidi shuleni hapo, kwani
akishachapwa fimbo kadhaa za mkononi, baadae inakuwa vigumu kwake kufanya kazi
za nyumbani za kufua, kuosha vyombo na kupika.
Biashara
Hivi karibuni
alilazimika kuhamisha makazi yake na watoto kutoka eneo la Moshono, alikokuwa
akiishi na mumewe Shani Malepu na kuanza kuishi katika chumba cha uani kwenye
jengo ambalo amefungua biashara yake ya duka mjini Arusha.
“Kule Moshono ni
mbali sana na shule na ilikuwa inatugharimu nauli za kila siku ili kuwahi
masomo na mara nyingi tulikuwa tunachelewa kufika shuleni,” alielezea Aisha.
Mama huyo ana matarajio ya kuendelea na elimu ya sekondari na anasema kuwa
Mungu akimsaidia basi angependa kufika hadi chuo kikuu kabisa.
“Mimi binafsi nina
juhudi katika elimu, maana nilianza shule nikiwa tayari najua kusoma maana
nilikuwa najifunza mwenyewe nyumbani huku nikiendelea na biashara zangu kama
kawaida,” anasema.
Mume
Akizungumza na
gazeti hili, mume wa Aisha, Malepu alisema haoni tatizo kwa mama wa watoto wake
kusoma shule ya msingi na wanawe. “Ni uamuzi wake mwenyewe na anaonesha kupenda
shule.
Tuliwahi kupanga
kuwa ajiunge na vyuo vya ufundi stadi, lakini baadaye akaona ni vyema zaidi
ajiunge na elimu ya msingi na ninadhani ana mpango wa kuwa mwalimu baadaye,”
alisema.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment