MAHAKAMA ya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, imemtia
hatiani na kumhukumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kwenda jela
mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni moja, kutokana na kesi iliyokuwa
ikimkabili ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo iliyohudhuriwa na wabunge wengi wa
Chadema, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa, alisema mahakama imemkuta
Mbowe na hatia, hivyo kutakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa
faini kiasi cha Sh milioni moja.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, katika kesi hiyo
ya jinai namba 73 ya mwaka 2011, alidaiwa kumshambulia Nassir Yamin, katika
Kijiji cha Nshara, kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai, katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010.
Mpelembwa alisema mahakamani hapo kuwa hukumu iliyotolewa
mahakamani hapo imezingatia ushahidi uliotolewa kwa upande wa mlalamikaji
Nassir Yamini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe akizungumza
mahakamani hapo, alisema hukumu iliyosomwa mahakamani hapo haijamtendea haki.
Alisema kesi yake hiyo haikustahili kuchukua muda mrefu kama
mahakama ilivyofanya kwa kuchukua zaidi ya miaka mitano bila kusomewa hukumu.
Hata hivyo, Mbowe amelipa kiasi cha fedha Sh milioni moja
alichotakiwa kulipa kama hukumu ilivyoeleza, kwa kumtaka kulipa kiasi hicho cha
fedha au kwenda jela mwaka mmoja.
Lema na Polisi
Wakati Mbowe akihukumiwa, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema jana alishindwa kuzuia hasira zake na kutaka kupigana na mmoja wa askari
polisi katika kituo cha kuandikisha wapigakura cha Mkombozi kata ya Sokoni One,
Jimbo la Arusha.
Tafrani hii ilitokea baada ya kukuta polisi huyo akiandikisha
wananchi wanaohitaji vitambulisho, kabla ya kuingia ndani ya chumba cha
waandikishaji.
Vurugu hizo zilitokea saa 5:30 asubuhi, mara baada ya Lema
kuingia eneo hilo akitembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura kuangalia hali
halisi.
Alipofika kwenye kituo hicho alikuta mmoja wa Polisi akiwa
amevaa kiraia (Jina halikupatikana mara moja), akiwa na daftari dogo
akiorodhesha majina ya wapiga kura kwa lengo la kupunguza foleni.
Akizungumza na wananchi huku Lema akiwa amezungukwa na askari
polisi, alisema huo sio utaratibu wa kufanywa na polisi na hata Tume hairuhusu
Polisi kufanya kazi hiyo bali kulinda amani tu.
Hata hivyo, Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha, Thomas
Maleko, akimtuliza hasira Lema akisema wao wanafanya kazi hiyo, ili
kuwapunguzia adha wananchi ambao wanafika kituoni saa 9:00 usiku, hadi siku ya
pili wanakaa kutwa nzima bila kupata fursa ya kuingia chumba cha kujiandikisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, ndipo Polisi walipoamua kuandikisha
watu kwa makubaliano na waandikishwaji wenyewe, ili waondoke nyumbani wakafanye
kazi zingine na kesho yake wakirejea wanapata fursa hiyo.
“Hawa watu hata wakikaa hapa hawawezi kuingia ndani ya chumba
husika, maana kuna kompyuta moja tu, hivyo wanapigwa na jua, hivyo utaratibu
huu sisi tumeona ni mzuri, tunaandika jina la mtu kisha tunamruhusu aende
nyumbani hadi kesho aje anaingia ili kupata kitambulisho,” alisema.
Hata hivyo, licha ya maelezo ya polisi, Lema hakukubaliana
nayo na kuwasiliana na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd ambaye alimtuma
Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, ambaye naye hakutaka kuzungumza chochote na
waandishi wa habari na pia hakutaka kutaja jina lake.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment