Makada wa CCM, wameendelea kupigana vikumbo katika ofisi
za makao makuu ya chama hicho mjini hapa kwa ajili ya kuchukua fomu za kuomba
kuteuliwa kugombea urais. Jana ilikuwa zamu ya Balozi Augustine Mahiga na
Monica Mbega aliyejitosa kimya kimya.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu yake, Balozi Mahiga
alisema nchi imekuwa katika hatari ya kupoteza umoja jambo ambalo linahitaji
kutazamwa upya na kuimarishwa ili iendelee kuwa na amani.
“Hakuna muungano wa nchi mbili uliowahi kudumu kama wetu.
Nimesafiri kwenda nchi mbalimbali duniani na kuulizwa siri ya muungano huu
kudumu hadi leo,” alisema.
Alisema akifanikiwa kuingia Ikulu, ataendeleza tunu hiyo
ya Taifa.
Balozi Mahiga alisema kuwa Taifa limeanza kulegalega
kutokana na rushwa na ufisadi.
“Tusiposhughulika na matatizo haya, Taifa
linaweza kuyumba na kupoteza mwelekeo,” alisema.
Alisema tatizo hilo linaweza kumalizwa kwa viongozi
kushirikiana na wananchi.
Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, ripoti ya Mkaguzi na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), imeonyesha kuwapo na upotevu wa mabilioni
ya fedha kila mwaka.
Hata hivyo, alisema CAG na Bunge wamekuwa wakipiga
kelele, lakini wanaofanya matendo hayo bado wanadunda.
Alipoulizwa atawezaje kuiongoza Tanzania wakati yeye
alikuwa nje ya nchi kwa muda mrefu alijibu: “Kama balozi unashindwa kuelezea
kilichotokea nchini kwako hufai kuwa balozi…Uongozi wa kimataifa niliupata,
sasa naurudisha nyumbani ili kuiunganisha Tanzania na mataifa mengine,”
alisema.
Mbega: Nitaendeleza yaliyofanywa na JK
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Monica alisema kuwa
endapo atafanikiwa katika kinyang’anyiro hicho, atatekeleza Ilani ya chama na
kuendeleza mambo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya nne.
‘Nitaangalia changamoto gani ambazo hazikuweza kuleta
maendeleo na kuzishughulikia,” alisema. Mbega alisema atafanya hivyo kwa
kutumia wataalamu wa ndani ya nchi. Nitatumia watalaamu wa kila aina katika
kuiendeleza Tanzania, alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment