SERIKALI imekiri kuruhusu uanzishwaji wa kiwanda cha
kusindika nyama ya punda kilichopo mkoani Dodoma.
Imekiri hivyo baada ya Mbunge
wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), kuibua hoja hiyo juzi jioni wakati wa
kupitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa
fedha 2015/2016.
Katika hoja yake, alitaka kujua juhudi zilizofanywa na Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA), kukagua viwanda vya usindikaji wa chakula ikiwa ni pamoja na kiwanda hicho.
Aliilaumu Serikali kukaa kimya
bila kutoa taarifa za kiwanda hicho ambacho mwekezaji wake ni raia wa kigeni
kutoka China, huku akihoji iwapo nyama hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Alisema uzalishaji wa nyama
hiyo licha ya kuashiria kutoweka kwa wanyama kazi hao, lakini pia unaweza kuzua
hofu ya kiimani miongoni mwa jamii kutokana na nyama hiyo kuingizwa sokoni.
“Sasa hivi kuna kiwanda hapa
nchini kinachakata nyama ya punda, ipo hatari ya hawa punda virongwe (wanyama
kazi) kuadimika kwa kuwafanya kitoweo,” alisema Rajab.
Hata hivyo, aliishangaa Serikali kuruhusu kiwanda hicho bila kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na matumizi ya nyama hiyo.
“Mimi napata wasiwasi mkubwa
kuhusiana na nyama hii, kwanza uzao wa punda ni mdogo, sasa kuwavuna kwa ajili
ya kitoweo kunatishia wanyama hawa kutoweka.
“Lakini hata hivyo mimi nashangaa, hapa Tanzania tunao ng’ombe wengi, mbuzi, kondoo na kuku wa kutosha tumeshindwa kuwekeza katika mifugo hii halali hadi tuanze kuchinja punda ndiyo uwekezaji uliofika huo?” alihoji.
“Lakini hata hivyo mimi nashangaa, hapa Tanzania tunao ng’ombe wengi, mbuzi, kondoo na kuku wa kutosha tumeshindwa kuwekeza katika mifugo hii halali hadi tuanze kuchinja punda ndiyo uwekezaji uliofika huo?” alihoji.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa
Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titas Kamani, alikiri uwepo wa kiwanda hicho
na kusema kuwa nyama hiyo imepimwa na wataalamu na haina madhara kwa binadamu.
Alisema nyama ya punda
inayozalishwa katika kiwanda hicho inasafirishwa nje ya nchi na haitumiki kwa
mahitaji ya soko la ndani.
“Hapa kati kati kulikuwa na
wimbi kubwa la wanyama kazi hawa kusafirishwa kwenda Kenya huko kuna viwanda
hivi, sasa tulioana bora tuwachinje na kuwasindika wenyewe kisha tuuze nyama
tupate fedha,” alisema Dk. Kamani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema wizara yake kupitia TFDA
imefanya uchunguzi na kujiridhisha kuhusiana na ubora wa nyama hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge jana, Naibu Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Uvuvi,
Kaika Telele, alisema mahitaji ya soko la nje ndiyo yaliyoisukuma Serikali
kuruhusu kiwanda hicho.
“Mwanzo sisi tulikataa kwa sababu uzao wa punda ni mdogo, kwa hiyo tuliona mazingira ya wanyama hawa kutoweka ni mkubwa.
“Taarifa za kwanza ilikuwa punda takriban 200 walikuwa wanachinjwa kwa sasa sijui ni wangapi, baadaye tuliona kama hilo soko lipo nje ya nchi na hiyo fedha ipo, kwanini tusifanye wenyewe,” alisema Telele.
No comments:
Post a Comment