Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kushoto) akizungumza na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alipokwenda kumjulia hali katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam jana. |
Kauli ya Gwajima
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima
alisema alipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki
dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili ya kumlinda, lakini
wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka kumtorosha.
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza
kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata
tatizo akiwa mikononi mwao.
“Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu
kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani,
ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi
ili likitokea lolote niweze kujilinda,” alisema Gwajima.
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji wake na kuchukua
silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu
umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa
kinachodaiwa kuwa nilitaka kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza
na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha
ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi
alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika vyombo vya habari
kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya
mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu
kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali
ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
Makonda amtembelea
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye alikuwa
amemwandikia Gwajima barua akimwita ofisi kwake, jana mchana alimtembelea
hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali kiongozi huyo lakini akasisitiza
kuwa nia yake bado ipo palepale.
“Nilimtaka leo aripoti ofisini kwangu lakini kwa bahati
mbaya anaugua na amelazwa. Nitakwenda kumuona ili nijue hali yake ikoje,”
alisema Makonda kabla ya kufunga safari kwenda hospitali alikolazwa.
Alisema pia atataka kiongozi huyo wa kiroho amweleze
anavyoelewa maana ya uhuru wa kuabudu unaoelezwa katika Katiba, usajili wa
taasisi yake na katiba ya taasisi hiyo. “Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye
wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema
Makonda.
Maaskofu wahoji mambo manne
Wakati huohuo; maaskofu na wachungaji kutoka makanisa
mbalimbali wametoa tamko wakihoji maswali matatu kuhusu tukio lililompata
Askofu Gwajima.
Akitoa tamko hilo, Askofu wa Kanisa la Pentekoste Agizo
Kuu, Dk Mgullu Kilimba alisema wanajiuliza ilikuwaje Gwajima aende akiwa mzima
atoke akiwa mahututi?
“Tumeshindwa kuelewa nini kimempata mwenzetu huyu.
Tunajiuliza je, vyombo vya usalama vimekuwa siyo sehemu salama kama zamani?”
alihoji.
Kuhusu tuhuma za kutoroshwa kwa Gwajima, maaskofu hao
wamehoji: “Kama alikuwa anaona ugumu wa kutoroka akiwa mwenye afya tele,
itakuwaje rahisi kutoroshwa akiwa mahututi na kwenye ulinzi mkali wa polisi?”
Pia walihoji kuhusu mlalamikaji wa kesi dhidi ya Gwajima
aliyetajwa kwa jina la Aboubakar,
wakisema si mtu sahihi kwa sababu hawezi kuonyesha ameumizwa kiasi gani
na matamshi ya Gwajima. Hata hivyo, Kova alisema hawamtambui mtu huyo wala
hajui lolote kuhusiana na mlalamikaji huyo aliyetajwa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment