Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amesema, amemsamehe Askofu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima ambaye hivi karibuni alimtolea maneno makali kutokana
na kutofautiana naye juu ya msimamo wa viongozi wa Kikristo kuhusu Katiba
Inayopendekezwa.
Kardinali Pengo alitoa msamaha huo mbele ya waumini
katika Kanisa la St Joseph, Dar es Salaam jana, siku mbili baada ya Askofu
Gwajima kuhojiwa na Polisi kwa madai ya kumkashifu kiongozi huyo, mbele ya hadhara.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa kauli za kumkashifu
kiongozi huyo kwamba amewasaliti wa viongozi wenzake wa Kikristo kwa kuwataka
waumini wa dini hiyo kuamua wenyewe suala la Katiba Inayopendekezwa kinyume na
msimamo wa waraka wa kupinga katiba hiyo uliotolewa na Jukwaa la Wakristo
Tanzania (CCT).
Baada ya kutolewa kwa waraka huo ulioagiza waumini
kuipigia kura ya hapana katiba hiyo, Askofu Pengo alinukuliwa akisema viongozi
wa dini hawana mamlaka ya kuzuia wananchi kuikubali Katiba hiyo huku akisisitiza
waachiwe uhuru wao wa kuamua.
Akizungumza jana wakati wa ibada ya Jumapili ya Matawi,
inayoadhimishwa wiki moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, Kardinali Pengo, bila ya
kumtaja jina alisema: “Natumia nafasi hii kueleza juu ya maneno ambayo
yalitolewa na mchungaji fulani, sikumbuki anaitwa nani… nasema nimemsamehe
kutoka ndani ya moyo wangu wote, anaweza kuwa na sababu zake ila nimemsamehe
kabisa.
“Sina ghadhabu wala chuki ila kinyume chake, naomba
tumwombee yeye na watu wote waliokuwa wamehusika pengine nyuma yake ili Mungu
aweze kutulinda na kutudumisha katika hali ya amani ya Taifa letu.”
Alisema hatua ya Polisi kumkamata ni sehemu ya kutekeleza
utaratibu wa jeshi hilo tu, lakini yeye kwa nafsi yake ameshamsamehe.
Atolewa ICU, wafuasi wakamatwa
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima ametolewa kwenye
chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kuhamishwa katika
wodi ya kawaida baada ya afya yake
kuendelea vizuri.
Askofu huyo alikuwa ICU kwenye Hospitali ya TMJ,
Mikocheni, alikofikishwa usiku wa Ijumaa baada ya hali yake kubadilika ghafla
alipokuwa akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo akiitikia wito wa
polisi uliomtaka kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya
Kardinali Pengo.
Akizungumza jana, mke wa Askofu huyo, Grace Gwajima
alisema baada ya madaktari kumuona anaendelea vizuri, wameamua kumtoa ICU na
kumpeleka kwenye wodi ya kawaida.
“Tunamshukuru Mungu sasa hivi anaendelea vizuri tofauti
na alivyokuwa jana (juzi) alikuwa hawezi kula chakula na kuongea lakini sasa
hivi anaongea na anakula chakula,” alisema na kuongeza:
“Tunashangazwa ni nini kimetokea Polisi wakati akihojiwa.
Alitoka nyumbani akiwa mzima na ametolewa polisi akiwa amebebwa hajitambui.”
Mke wa Askofu huyo alisema wakiwa hospitalini hapo usiku
wa kuamkia leo, walikuja askari polisi na kuwakamata baadhi ya viongozi na
walinzi wa kanisa hilo na kuchukua magari yao.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema inawashikilia na kuwahoji watu 15 ambao
wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu
Gwajima.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kamanda
Kova alisema jana saa 9.30 usiku watu hao 15, katika hali isiyo ya kawaida
walifika hospitalini hapo wakidai kwamba walikuwa wanataka kwenda kumuona
mgonjwa huyo.
“Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia shaka
hivyo waliwakatalia kuingia. Kundi hilo la watu 15 lilijaribu kutumia nguvu
kuingia katika chumba alicholazwa Askofu Gwajima lakini walikamatwa na kikosi
maalumu cha Polisi ambacho kabla ya tukio hilo kilikuwa kinafuatilia mwenendo
wa kundi hilo.”
Alisema baada ya kukamatwa, watuhumiwa hao walipekuliwa
hapohapo TMJ na kukutwa na begi ambalo lilikuwa na vitu mbalimbali mojawapo
vikiwa ni bastola aina ya Berreta ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za bunduki
aina ya Shortgun, vitabu viwili vya hundi na hati ya kusafiria yenye jina la
Gwajima Josephat Mathias.
Alisema baada ya upekuzi kukamilika, watuhumiwa
walifikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja
na kupata uhalali wa wao kumiliki silaha hizo na risasi.
“Upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni ya
kubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka
kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.”
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment