Hali ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima inaendelea vizuri, ingawa haijabainika anasumbuliwa na tatizo gani
kiafya hadi hapo vipimo vitakapopatikana.
Gwajima aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu kwenye Hospitali ya TMJ, Mikocheni, Dar es Salaam alifikishwa
hospitali hapo juzi usiku baada ya hali yake kubadilika ghafla alipokuwa
akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo juzi mchana
akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa
lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo jana, Dk
Fortunatus Mazigo anayemtibu kiongozi huyo wa kiroho alisema kuwa hali yake
haijabadilika tangu afikishwe hospitalini hapo jana (juzi) usiku.
Alisema hadi sasa bado hawajafahamu ana tatizo gani
kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya vipimo, ingawa kuna matumaini kutokana
na kuwa na hali nzuri katika mfumo mzima wa damu, mapigo ya moyo na viungo
vyote vinafanya kazi.
“Sina cha kusema kuhusu ugonjwa wake kwa sababu hiyo ni
siri ya anayeumwa na daktari, ninachoweza kusema hali yake aliyokuja nayo jana
usiku haijabadilika, ingawa kuna matumaini kwa sababu vitu muhimu vipo sawa,”
alisema Dk Mazigo.
Hali ilivyo hospitalini hapo
Waumini kutoka katika Kanisa na Ufufuo na Uzima walikuwa
wakipishana hospitalini hapo jana ili kumwangalia kiongozi wao ambaye amelala
kitandani, akiwa hawezi kuzungumza.
Mchungaji Yekonia Biyagaze ndiye anafanya kazi ya ziada
kuhakikisha waumini wanaoshindwa kupata nafasi ya kuingia wodini kumwona
kiongozi wao wanapata maelezo ya kina kutoka kwake kuhusiana na kinachoendelea
kwa mgonjwa huyo.
Baadhi ya waumini waliozungumza na gazeti hili
hospitalini hapo, walieleza kushtushwa kwao.
Muumini aliyejitambulisha kwa jina la Masinde alisema
kuwa anachofahamu kiongozi wake alikuwa Arusha na alirudi ili kutii amri ya
polisi ya kutakiwa kufika kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
“Nimeshtuka, natamani ufanyike uchunguzi wa kina tubaini
nini kinaendelea ni kiongozi mkubwa na ni muhimu kwetu kama waumini wake,
sitarajii kama litatokea jambo baya, kwani inaweza kuwa hatari,” alisema
muumini huyo.
Masinde alisema walikuja wengi, lakini baada ya kupewa
maelezo na Mchungaji Biyagaze wakaamua kuondoka ili kupisha na wengine wapate
nafasi ya kumjulia hali kwa sababu kila mmoja anataka kusikia au kuona kwa
macho badala ya kuambiwa akiwa mbali.
Awali, kabla ya kufika katika wodi hiyo kulikuwa na
askari kadhaa waliovaa kiraia waliozunguka eneo hilo kwa kupanda juu ghorofani
alipo Askofu Gwajima na kushuka, ambapo baada ya muda walipungua na kubaki
wachache.
Kabla ya kuingia chumba cha mgonjwa
Tofauti na ilivyozoeleka kuwa unapotaka kuingia chumba
cha mgonjwa mnapewa maelekezo na daktari, katika kile kinachoonekana
kuhakikisha usalama unakuwapo.
Aliyekuwa na jukumu la kutoa maelekezo kwa watu wote
wanaokwenda kumwona mgonjwa, wakiwamo wanahabari ni Mchungaji Biyakaze, ambaye
aliwataka wakiingia ndani wasishike kitanda, wala shuka kwa usalama wao.
Hata baada ya kuingia, kundi la watu Askofu Gwajima
hakufumbua macho wala kupepesa, hali inayoonyesha kuwa bado yupo katika hali
isiyoridhisha.
Akiwa amelala chali, huku amefungwa mashine ya kupimia
mapigo ya moyo mkononi, chumbani humo kulikuwa na muuguzi aliyekuwa anaratibu
kila kinachoendelea, ikiwamo kuwazuia watu wasiguse kitu chochote.
Kabla ya kuingia ndani na kumwona mgonjwa, Mchungaji
Biyakaze alizungumzia hali ya mgonjwa alisema anaendelea vizuri, ingawa
alishindwa kumalizia na kubaki akisema...lakini na kumalizia kusema kuwa
kinachonipa moyo wa kuwa atapona kwa sababu ni mtumishi wa Mungu sina jingine.
Mlangoni mwa wodi alimolazwa Askofu Gwajima kulikuwa na
watu ambao hawatoki muda wote, mmojawao alipopewa pole alisema kuwa asipewe
pole kwani huo ni ushindi na hakuna mapambano yasiyokuwa na vikwazo.
“Usinipe pole, nipongeze huu ni ushindi na ndiyo
mapambano yalivyo lazima kuwe na vigingi, ambavyo ukivivuka unakuwa umeshinda
na sisi tumeshinda,” alisema kijana huyo.
Slaa, Baregu wafika hospitalini
Saa sita mchana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad Slaa alifika hospitalini hapo akiongozana na
Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu kumwona Gwajima.
Baada ya kumwona mgonjwa, Dk Slaa alizungumzia utata
unaowapata watu wanaohojiwa na polisi, huku akisisitiza kuna vitu vinatakiwa
kufanyiwa kazi, ikiwamo kubaini kuna nini.
Alisema sheria za kuhojiwa zipo wazi kuwa mtu asihojiwe
zaidi ya saa nane, vitu kama hivyo vinatakiwa kuzingatiwa katika mahojiano.
“Nyinyi kama waandishi ndiyo kazi yenu kuangalia kwa
undani kuna nini kinaendelea katika haya mahojiano hadi mtu anapoteza fahamu,
siyo huyu hata kama kuna mwingine ilimtokea hali hiyo,” alisema Dk Slaa.
Akizungumza hali ya mgonjwa kwa mtizamo wake, alisema
kuwa daktari anayemtibu hawajawafahamisha nini kimempata, lakini kwa bahati
mbaya hata mgonjwa mwenyewe hawezi kuzungumza na wao hawakuweza kumuuliza
chochote, hivyo hana la kusema.
“Angekuwa anazungumza, labda angeniambia ilikuwaje,
lakini hawezi hivyo sijapata lolote kutoka kwake wala daktari,” alisema Dk
Slaa.
No comments:
Post a Comment