Serikali itawasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Makosa
ya Mtandao wa mwaka 2015 kwa hati ya dharura unaoorodhesha adhabu mbalimbali,
ikiwamo ya faini ya Sh50 milioni au kifungo kisichopungua miaka saba kwa mtu
atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao, kuchapisha
taarifa yoyote ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uongo na matusi ya
kibaguzi.
Sheria hiyo katika Kifungu cha 48 inaipa Mahakama mamlaka
ya kutaifisha mali iliyopatikana kutokana na kosa lililofanywa na mhusika.
Sheria hiyo pia itawataka wote watakaobainika kufanya makosa hayo kuwasilisha
hati zao za kusafiria kwa mamlaka husika hadi hapo watakapolipa faini au
watakapokuwa wamemaliza kutumikia vifungo.
Muswada huo ambao ukipitishwa utakuwa sheria,
unawasilishwa bungeni katika kipindi ambacho kina matukio mengi ya watu
kusambaza picha za ngono na utupu mitandaoni, kuingilia mawasiliano ya kompyuta
ya watu wengine bila ridhaa yao.
Pia, kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu atakayebainika
kusambaza picha za ngono, uasherati na matusi, atatozwa faini isiyopungua Sh30
milioni au kwenda jela miaka 10, mtu atakayesambaza picha za utupu atalipa
faini isiyopungua Sh20 milioni au kwenda jela miaka saba.
Inawabana pia watoa taarifa za uongo. Katika Kifungu cha
16, inasema mtu atakayetoa taarifa, takwimu au maelezo kwa njia ya picha au
maandishi au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo, akipatikana na hatia
atalipa faini isiyopungua Sh3 milioni au kifungo kisichopungua miezi sita.
Kuhusu mauaji ya kimbari, inakataza mtu kuchapisha au
kusababisha kuchapisha vitu vinavyochochea au kuhalalisha matendo
yanayosababisha mauaji ya kimbari na adhabu yake ni faini ya Sh10 milioni au
miaka mitatu jela .
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment