Siku chache baada ya baba aliyedaiwa kubaka
watoto wake wawili wakazi wa wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani kutiwa
mbaroni na polisi, mama wa watoto waliokuwa wakitendewa unyama huo ameanza
kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya
ndugu wa mume wake.
Mama huyo alisema kuwa baada ya
ndugu wa mume wake kupata taarifa ya kukamatwa kwa ndugu yao wameanza kumtisha
ikiwamo ya kutishiwa kuondolewa eneo analoishi
na kususiwa kuhudumiwa watoto
wake.
Kutokana na vitisho hivyo mama huyo ameomba msaada
serikalini ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kutokana na vitisho
anavyopokea kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa.
“Nasikia uchungu sana, bado watoto wangu ni wadogo na
wote bado wanasoma, tegemezi kuu mimi, naomba wadau wanisaidie nikiendelea
kutishiwa na pia nisaidiwe waendelee
kupata elimu, kwa sasa baada ya tukio hili nitakwama kiuchumi maana mtaji
umekwisha kwa siku hizi nne tangu tukio limegundulika sijaweza kwenda kwenye
biashara zangu za mboga mboga nasimamia familia na hili suala bado tunaendelea
nalo polisi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema
ofisi yake imepata taarifa za mama huyo kupata vitisho kutoka kwa ndugu wa
mtuhumiwa na kwa sasa jeshi hilo
inalifuatilia kwa karibu zaidi ili kuweza kuwabaini wahusika na watakamatwa na
kufikishwa kwenye vyombo husika.
“Hao ndugu
wanaomwambia huyo mama kafanya kosa kwenda kuripoti kituo cha polisi wanakosea sana, maana tukio lenyewe ni la
kinyama sana, miaka zaidi ya miwili baba mzazi anawatumia watoto wake tena
wadogo kinyumba wao wanaona ni jambo dogo, sasa tunawafuatilia hao na
tukiwabaini nao tutawashughulikia,” alisema Matei.
Alisema, “Taarifa imeshakuwa ipo wazi na majibu ya
daktari yameshaonyesha wale watoto wamefanyiwa kitendo kibaya na zaidi wameharibiwa
kiasi kwamba inasemekana kama wangeendelea zaidi kufanyiwa unyama huo wangeweza hata kupoteza maisha,kwa hiyo huyo
mama alikua sahihi kusema na angesemea wapi zaidi ya kituoni, kwa hiyo
tutawasaka hao ndugu wanaomtishia huyo mama tuwachukulie hatua.”
Naye mwalimu mkuu Shule ya Msingi Miembe, Saba Rajab
Chalamila anakosoma mmoja wa watoto hao waliobakwa na katibu wa watoto waishio
katika mazingira magumu Mtaa wa Miembe Saba wamesema kwa sasa wanaangalia
uwezekano wa kumsaidia binti huyo kupata vifaa vidogo vidogo vya darasani kama
kalamu na madaftari wakati huu na anajiandaa na mitihani ya kumaliza elimu ya
msingi.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment