ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
jana alizimia na kisha kukimbizwa hospitali wakati akihojiwa Kituo Kikuu cha
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Gwajima ambaye alijisalimisha kituoni hapo saa 8:22 jana
mchana akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufika kutokana na tuhuma za kutoa
lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Waandishi wa Mtanzania Jumamosi waliokuwa kituoni hapo
wanaeleza kuwa walimuona Gwajima akitolewa kutoka katika chumba cha mahojiano
akiwa amebebwa.
Kwa mujibu wa waandishi hao Gwajima ambaye alikuwa
amebebwa na maofisa wa polisi alipelekwa moja kwa moja kwenye gari aina ya Noah
kwa ajili ya kumpeleka hospitali.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa 3:16 usiku lilikuja
katika kipindi kisichozidi dakika saba tangu askofu huyo alipoonekana akiwa
ameshikiliwa na wasaidizi wake kuelekea msalani huku yeye mwenyewe akiwa
amejishika kichwa.
Wakati akipelekwa hospitali, msafara wake ulikuwa ni wa
magari mawili mojawapo likiwa ni aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za
usajili PT 1848 na Noah yenye namba za usajili T 215 BEM.
Akizungumza na gazeti hili kituoni hapo, mwanasheria wa
askofu huyo, John Mallya alisema wakati wakiwa katika mahojiano, alisema
anahisi kizunguzungu na baadaye akaishiwa nguvu na akawa amefumba macho.
Mallya alisema baada ya hali hiyo kutokea, polisi
walimchukua na kisha kumpeleka katika hospitali ya Jeshi la Polisi iliyoko
Kurasini, Dar es Salaam.
Wakati Mallya akiwasiliana na gazeti hili majira ya 4:30
usiku alisema kuwa walikuwa wakifanya mchakato wa kumuhamishia katika hospitali
ya TMJ kutokana na yake kutokuwa nzuri.
“Siwezi kujua tatizo ni nini na siwezi kuzungumza
chochote kuhusu hilo maana hayo ni mambo ya kitabibu” alisema Malya.
Ilipotimu saa 4:41 Waandishi wa gazeti hili ambao nao
walifika katika hospitali hiyo ya Jeshi la Polisi walishuhudia Gwajima akitolewa
katika hospitali hiyo ya Jeshi la Polisi na kisha kupakizwa katika gari maalum
la kubebea wagonjwa lenye namba DFP 6309.
Wakati hayo yakitokea taarifa nyingine zilizolifikia
gazeti hili zilidai kuwa; kwa muda wote akiwa katika mahojiano, Gwajima alikuwa
hajala chochote hali ambayo iliibua wasiwasi kwamba huenda ilichangia
kubadilika kwa afya yake.
Polisi mmoja aliyekuwa katika chumba cha mahojiano
aliwaeleza waandishi wetu kwamba Askofu Gwajima alipoteza fahamu muda mfupi
baada ya kuhojiwa kuhusu mali anazozimiliki.
Awali wakati Gwajima alipowasili kituoni hapo mchana
kabla ya kuhojiwa alizungumza na waandishi wa habari ambapo alikiri kutoa lugha
chafu dhidi Kardinali Pengo.
Gwajima ambaye alifika kituoni hapo saa 8:22 mchana
alisema kauli yake hiyo ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii aliitoa
kutokana na Kardinali Pengo kuwageuka wenzake ambao ni Baraza la Maaskofu
Tanzania linalounganisha Wakatoliki, Pentekoste na Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT) kukubaliana kwa pamoja kuwa hawataki Mahakama ya Kadhi.
Alisema maaskofu wote walikubaliana kuhusu tamko hilo na
kisha kulisaini lakini anamshangaa Kardinali Pengo ambaye pia alisaini
kuwageuka.
“Mimi kama kiongozi wa kiroho nikaona nimkemee kiongozi
mwenzangu wa kiroho aache mambo ambayo si mazuri. Hakuna maneno ya kashfa
ambayo nimeyatoa. Niliyotoa ni neno la Mungu linalotumiwa kumwongoza mtumishi
wa Mungu,” alisema Gwajima.
Alisema anashangaa kuitwa polisi kwani hajatukana polisi
na ndio sababu akaitika wito na kufika.
Gwajima alifika polisi akitembea kwa miguu kutokana na
foleni kali iliyokuwepo barabarani huku akiwa ameongozana na Mwanasheria wake
John Malya pamoja na baadhi ya wachungaji, waumini wa kanisa hilo na wengine
waliotajwa kuwa ni walinzi wake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna
Suleimani Kova alisema Mchungaji Gwajima ametii amri ya Jeshi hilo kama
alivyotakiwa.
Kova alisema baada ya kufika kituoni hapo alielekezwa
kwenda kumuona Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Costantine
Massawe.
Akitaja tuhuma zinazomkabili Mchungaji Gwajima, Kova
alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana hadharani kiongozi wa Kanisa
Katoliki Kardinali Pengo.
“Taratibu za kuhojiwa zimeshaanza kwa mujibu wa sheria na
mtuhumiwa atapewa haki zote anazostahili ikiwemo kuwa na ndugu yake wa karibu,
rafiki anayemwamini au wakili wake. Kama ilivyokawaida utakusanywa ushahidi
kutoka pande zote za shauri hilo ili kubaini ukweli wa jinsi tukio hilo
lilivyotokea,” alisema Kova.
Kova alisema baada ya hapo hatua nyingine za kisheria
zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya kitaalamu na ya kisheria ili
kuhakikisha kwamba haki inatendeka.
“Ili ufanisi upatikane katika upelelezi wa shauri hili ni
muhimu kupata ushirikiano kutoka kwa kila atakayetakiwa kulisaidia Jeshi la
Polisi kukamilisha haraka upelelezi wa shauri hilo ambalo limepata mvuto mkubwa
kwenye jamii,” alisema Kova.
Katika video na sauti zilizosambaa kwenye mitandao ya
kijamii hasa What’s App, Gwajima alirekodiwa akiwa kwenye ibada ya kanisa lake
akitumia lugha zisizokuwa na staa kwa Kardinali Pengo akimtuhumu kuwa ni
msaliti kwani amekwenda kinyume na Taasisi ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) na Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT) kwa kuwataka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa
kisha wapewe uhuru wa kupiga kura ya “ndiyo” au “hapana” tofauti na vyombo
hivyo vyenye dhamana ya kuongoza dini ya Kikristo vilivyotaka waumini waipigie
kura ya “hapana”.
No comments:
Post a Comment