JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,limemtaka
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
kujisalimisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo
la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo.
Hatua hiyo ya polisi imekuja baada ya jeshi hilo kupokea
malalamiko, ambapo inadaiwa Mchungaji Gwajima alitoa lugha ya kashfa dhidi ya
Kardinali Pengo ambaye alipinga tamko lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT) la kuipigia kura ya Hapana Katiba Inayopendekezwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi, Kamishna Suleiman Kova, imemtaka
Mchungaji Gwajima kujisalimisha haraka katika Kituo cha Polisi cha Kati kwenye
Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kashfa na
matusi.
Kova alisema jeshi hilo limepokea malalamiko ya
kukashifiwa na kutukanwa hadharani Kardinali Pengo.
Alisema matusi hayo yameonekana kupitia mitandao
mbalimbali ya kijamii ya WhatsApp na mingineyo, ambapo kuna sauti iliyorekodiwa
na picha za video zikimuonyesha Mchungaji Gwajima akimkashifu na kumtukana kwa
maneno makali Kardinali Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.
Kova alisema baada ya tukio hilo, juhudi mbalimbali
zimekuwa zikifanyika ili kumpata Mchungaji Gwajima bila mafanikio.
“Ni muhimu sana kwa Mchungaji Josephat Gwajima aripoti
mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na
nafasi yake katika jamii.
“Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri
hili unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Kova.
Sehemu ya maneno hayo ambayo yanamwonyesha Gwajima
akizungumza kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ni; “Pengo
unaaibisha kama mtoto mdogo aliyevaa pampasi aliyebebwa na mama yake, Pengo ni
mjinga asiyefaa, juzi aliokoka kwa kula chakula chake ovyo ovyo, sijui kala
maharage ya wapi?
“Pengo awe Mkatoliki amejishushia heshima yake mwenyewe,
aache uaskofu awe mkulima wa kawaida, hafai mzee ametudhalilisha kabisa na
amewageuka maaskofu wote kwa kile walichopatana .
“Amewadhalilisha maaskofu wote, amedhalilisha CCT,
amedhalilisha CPCT, pia amewadhalilisha Watanzania wote.”
GWAJIMA NI NANI
Gwajima ni mwasisi na mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima ambapo kwa sasa anaongoza waumini wapatao 70,000 kwa siku, na hivi sasa
yuko mbioni kuanzisha makanisa mengine mikoa yote ya Tanzania.
Kwa mujibu wa kauli zake alizopata kuzisema huko nyuma
katika moja ya mahubiri yake kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe
jijini Dar es Salaam, hivi sasa ana waumini wengi kuliko makanisa mengine
kutokana na huduma nzuri anayotoa kwa waumini na jamii kwa jumla.
“Nimefanikiwa kuwa na waumini wengi kuliko wengine kwa
sababu nahubiri Neno tu, sirushiani maneno na makanisa mengine.
“Sisi hatuna utamaduni wa kuwashambulia wachungaji
wenzetu. Wao hata wakitusema vipi, sisi tunakaa kimya kwani kujibishana
kunaleta mgawanyiko.”
GWAJIMA NA FLORA MBASHA
Februari 4, mwaka huu picha za mtoto mchanga zilisambazwa
katika mitandao ya kijamii na kudaiwa kuwa ni wa mwimbaji wa nyimbo za Injili
nchini, Flora Mbasha aliyezaa na Mchungaji Gwajima.
Hatua hiyo ilikuja miezi kadhaa tangu Flora aingie katika
mgogoro wa ndoa na mumewe Emmanuel Mbasha aliyefikishwa mahakamani kwa kosa la
ubakaji.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu taarifa za picha za mtoto
huyo, Mchungaji Gwajima alisema ni za uzushi na huenda zinasambazwa na mume wa
Flora, Emmanuel Mbasha.
Mchungaji Gwajima alikwenda mbali na kusema pamoja na
uzushi huo unaosambazwa dhidi yake kwa kuhusishwa katika uhusiano na Flora,
anamwachia Mungu kila kitu.
“Si unajua hiyo issue (suala, jambo) ya Mbasha ni ya muda
mrefu tu… wakati mwingine mimi huwa sijibu ujinga.
“Awali niliwaza kuwashtaki (alipoanza kuhusishwa kwamba
ana uhusiano na Flora) wanaoeneza uzushi huo, lakini nikaona ‘It doesn’t hold
water’ (haina mashiko), najua shutuma hizo zinatoka wapi,” alisema Mchungaji
Gwajima.
Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment