WAZIRI MKUU WA ZAMANI, FREDRICK SUMAYE |
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, imewataja
vigogo wanaohodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyaendeleza na kuwapa siku
90 kuhakikisha wanayaendeleza, kinyume
chake yatachukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tatu
Suleiman, ilisema vigogo hao walinunua mashamba katika eneo hilo na kisha
kuyaacha kwa muda mrefu bila kuyaendeleza akiwamo mke wa Waziri Mkuu Mstaafu,
Frederick Sumaye, Mama Ester Sumaye ambaye
anamiliki mashamba mawili, moja
likiwa na ukubwa ekari 145.5 likiwa na namba 6069 na 6070 na shamba la pili
lenye ukubwa wa ekari 103. 25 likiwa na namba 6071 na 6075, yote yakiwa
Misufini, Kibaha vijijini.
Taarifa hiyo inawataja watu wengine maarufu ambao
wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo kuwa ni,
Phillipo Marmo ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayemiliki
shamba 6159-6164 maeneo ya Kikongo, Nicodemus Banduka ambaye ni mkuu wa mkoa
mstaafu wa mikoa ya Pwani, Iringa na Mtwara anaye miliki shamba namba 1707 eneo
la Vikuge ambalo alilipata mwaka 2,000 na
Kipi Warioba aliyewahi kuteuliwa kugombea Ubunge Jimbo la Kawe ambaye
anamiliki eneo Mperamumbi lenye ukubwa wa heka 4000.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, watu wengi walichukua
mashamba katika eneo hilo kuanzia miaka ya 1986 na kushindwa kuyaendeleza na
kusababisha kuwa mapori hali iliyopelekea halmashauri hiyo kufuata sheria na
kanuni zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Kufuatia mashamba hayo kutelekezwa, halmashuri ya wilaya
hiyo inapanga kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara husika ili miliki zake
zifutwe endapo wahusika watashindwa kuyaendeleza kwa
muda waliopewa.
Tatu, alisema mwaka jana waliwataka watu wote waliochukua
mashamba hayo kuyaendeleza baada ya kufanyiwa uhakiki na baadhi ya watu
walijitokeza kuyaendeleza, lakini watu zaidi ya 40 hawajitokeza.
“Kutokana na kukahidi kuyaendeleza mashamba hayo,
tumeshapeleka majina ya wamiliki Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
na wizara imetutaka tutoe tena
siku 90 kama hawatatekeleza kwa kipindi hicho, watajua nini cha kufanya,’’
alisema.
Gazeti hili lilipowasiliana na Waziri Mkuu wa zamani,
Sumaye kwa njia ya simu ili kuzungumzia taarifa za mkewe kushindwa kuyaendeleza
mashamba hayo kwa kipindi kirefu, alisema hana taarifa zozote za mkewe
kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo anayomiliki.
‘‘Wewe ndiyo nakusikia, sisi hatujaliona hilo tangazo,
wala mke wangu hana hizo taarifa ila baadaye tutakapoziona tutakupigia simu
tuwasiliane,’’ alisema Sumaye.
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment