Mnenguaji mahiri na mkongwe nchini, Lilian Internet(35),
amesema vijana wengi walio katika fani hiyo wanajihusisha na matumizi ya dawa
za kulevya.
Nyota huyo, mzaliwa wa Mkoa Kilimanjaro, pia amelaani
tabia ya baadhi ya vijana kuwa na wapenzi wengi huku akisema anamshukuru Mungu
kwa kuwa ameweza kujiepusha na tabia hiyo na sasa ni mke wa mtu.
“Asilimia kubwa ya wanenguaji wanatumia dawa za kulevya,
si kwa sababu wanatumia dawa hizo ili wacheze vizuri jukwaaani, bali waliingia
huko kwa kufuata mkumbo. Jambo hilo silifurahii linaniumiza sana,” anasema
Internet.
Mnenguaji huyo ambaye jina lake halisi ni Lilian Josephat
Tungaraza anasema tatizo hilo ni kubwa na vijana wengi, hasa wasichana
wameangukia katika tabia hiyo kwa kudanganywa na wanaume na wakati mwingine wao
wenyewe kuwa watapata nguvu zaidi za kucheza jukwaani.
“Mimi nafanya vizuri na mashabiki wengi wanafurahia kazi
yangu tangu nilipojiunga na Bendi ya Twanga Pepeta mwaka 1997 ilipoanza. Mpaka
leo wengi wakiniona wanadhani nina miaka 20, lakini hii yote inatokana na
kujali afya yangu. Naomba Mungu awajalie ili watokane kwenye matumizi ya dawa
za kulevya kwani wengi wanadhalilika, hiyo inaniumiza,” anasema.
Lilian anasema mama yake ambaye ni mwenyeji wa Mwanga
mkoani Kilimanjaro, amekuwa na mchango mkubwa katika maisha yake kutokana na
kumuunga mkono kwa kazi anayoifanya, hivyo kusaidia kuwa naye karibu katika
mambo mbalimbali.
“Wakati wa kwenda kazini, kuna vyakula ninavyotakiwa kula
ambavyo sivitumii sana. Sina ulevi ninaotumia zaidi ya bia mbili kwa siku.
Vilevi vilivyokatazwa mimi situmii,” anasema.
Msanii huyo anaeleza kuwa hunywa baada ya kazi au wakati
mwingine akiwa nyumbani siku ya Jumatatu ambayo ni mapumziko kwake.
Akizungumzia mafanikio yake anasema: “Ni kujitunza kwa
sababu hii ni kazi ngumu. Kuna vitu unatakiwa kuwa unavifahamu na kutekeleza;
kwanza ni kulala mapema, kuwa na kiasi katika utumiaji wa pombe, lakini pia
kutokuwa na wanaume wengi kwani hiyo inakufanya pia upoteze mwelekeo.”
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Twanga Pepeta
International Asha Baraka anayesema: “Tumeona wasanii wengi wa Tanzania ambao
awali walikuwa wanafanya vizuri, lakini baada ya kujaa sifa na kukutana na
marafiki wengi hasa makundi, wakazama kwenye dawa za kulevya, sasa wanatapatapa
na kubaki kulaumu, wakati wenyewe wamejiharibia.”
Hata hivyo, Asha anasema Twanga Pepeta imekuwa ikitoa
mafunzo kwa wasanii ili kujiweka kando na matumizi ya dawa za kulevya kupitia
vikao vyao wakiwataka pia kuwa na nidhamu ya kazi.
“Nidhamu ya kazi ni jambo linaloingia katika haya yote.
Nimekuwa nikiwaashauri wasanii wangu katika haya na mara nyingi tumefanya hivyo
ndiyo maana unaona Twanga Pepeta imesimama mpaka leo, mengine yanatokana na
msanii mwenyewe kujibana katika makundi yasiyofaa,” anasema Asha Baraka.
Ushuhuda wa Diof
Mwanamuziki Msafiri Diofu anasema matumizi ya dawa za
kulevya yapo kwa wasanii wengi na wanaingizwa huko kutokana na makundi. Lakini
kwa upande wake, aliingizwa na rafiki ambaye hata hivyo ameshafariki.
“Uteja ni kitu kinachodhoofisha mwili. Nilikuwa siwezi
kupanda stejini kuimba kama sijabwia ‘unga’, nilikuwa mteja msafi. Kipindi cha
mwazo watu walikuwa hawajui kama mimi ni teja, ila wale wa karibu wakawa
wananiambia mbona sauti inabadilika kama inakwaruza na kukauka, hapo nikaanza
kushindwa kujichanganya na wanenguaji stejini,” anasema Diof na kuongeza:
“Ilifika wakati mwili ulidhoofu. Lakini Diofu huyu
unayemwona sasa ana afya, siyo kama nilivyoharibiwa na unga, nilishindwa
kujitegemea mwenyewe mpaka nilipopatiwa matibabu ya ‘methadone’.” Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment