RAIS Jakaya Kikwete ameamuru kubomolewa baadhi ya nyumba
zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba
za wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani, Ilala Dar es Salaam.
Akihutubia wananchi wa eneo hilo jana, Rais Kikwete
alisema nyumba hizo zitabomolewa pamoja na karavati hilo kupisha maji kupita na
kulijenga upya.
“Kwa sasa tunaendelea kuvuta maji yaliyojaa kwenye makazi
ya watu kwa kutumia pampu lakini baadaye itabidi tuvunje nyumba zilizoko juu ya
karavati kupisha ujenzi wa karavati jipya,” alisema.
Rais Kikwete ambaye alitembelea maeneo yaliyokumbwa na
kadhia hiyo jana, alisema wananchi wote watakaobomolewa nyumba zao watalipwa
fidia huku akitoa rai kwao kuacha tabia ya kujenga holela bila kuzingatia
matumizi ya eneo husika.
Katika hatua hiyo, alisema zipo taarifa za kuwapo uhitaji
wa chakula kwa waathirika na tayari uongozi wa wilaya na kamati ya maafa
zimeanza kushughulikia tatizo hilo.
Wananchi walioathirika na mafuriko hayo waliiomba
serikali kuharakisha hatua ya kutoa maji yaliyojaa kwenye makazi yao na kutoa
misaada inayohitajika.
Mvua inayoendelea kunyesha Dar es Salaam imesababisha
madhara makubwa vikiwamo vifo vya watu saba na nyumba zaidi ya 200 kuzingirwa
na maji katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment