Nyumba za wakazi wa bonde la Hananasifu kinondoni zikiwa zizungukwa na maji |
HALI ni tete katika jiji la Dar es Salaam,
kutokana na mvua ya masika iliyonyeshwa kwa siku tatu na kusababisha vifo vya
watu watano, huku nyumba nyingi zikiwa zimezingirwa na maji.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Buguruni kwa
Mnyamani na eneo la Jangwani katika Manispaa ya Ilala, ambako nyumba nyingi na
barabara zimeathirika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa nchini (TMA), mvua kubwa zaidi zinatarajia kuendelea kunyesha mpaka
Jumatano.
Kutokana na athari za mvua zinazoendelea
kunyesha, Mkuu wa Mko wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki (pichani) jana
aliongoza kikosi cha uokoaji katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani, ambako nyumba
250 zilizingirwa na maji, jambo ambalo vikosi vya uokoaji vililazimika kufanya
kazi ya kuwanasua watu waliokuwa wamekwama katika nyumba zao.
Uokoaji huo ambao mpaka jana jioni ulikuwa
ukiendelea, ulisaidiwa na wafanyakazi wa kampuni ya China Railway Jianchang
Engineering (CRJE), inayojenga Daraja la Kigamboni, kwa kutoa vifaa na
kushiriki katika uokoaji wa watu hao.
Sadiki alisema mpaka jana mvua hizo
zimesababisha vifo vya watu watano, akiwemo mtu mmoja aliyesombwa na maji,
mwingine aliyeangukiwa na ukuta na watatu ambao wamenaswa na umeme baada ya
nguzo ya umeme kuanguka Mbagala Mzambarauni katika Manispaa ya
Temeke.
“Wananchi wanatakiwa kuachana na tabia ya kutupa
taka ovyo katika maeneo ya mitaro, kwani ndiyo yaliyochangia maji kuleta
madhara, na walio mabondeni bado nawasihi kuondoka maeneo hayo,”
alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura alisema mtu mmoja ambaye hajatambuliwa mwenye umri kati ya miaka 45
hadi 50, anasadikiwa kusombwa na maji katika mto Goba.
Aidha, alisema katika eneo la Mwananyamala,
mlemavu wa viungo Edward Warioba (22) aliangukiwa na ukuta usiku wa kuamkia
jana akiwa amelala katika nyumba iliyokuwa imeingia maji na kulowanisha kuta
zake.
Wambura alitaka wananchi kuchukua tahadhari kwa
watoto wao na wahakikishe wanakwenda na kurudi kutoka shule wakiwa
salama.
Eneo la Jangwani, kati ya Magomeni na Faya
(Kariakoo), pia nyumba kadhaa zilizingirwa na maji huku baadhi ya wakazi wa
maeneo hayo wakihamia barabarani ili kujinusuru.
Lakini eneo la Jangwani, karibu na klabu ya
Yanga, walionesha kutokuwa na wasiwasi na mvua zinazoendelea kwa madai kuwa
hazijafikia kiwango cha kuwa na athari kwao.
“Kipimo chetu ni hiki hapa, (wanaonesha alama)
maji yakifika kimo hiki tunajua wakati wa kuhama nyumba zetu umewadia lakini
kwa sasa maji haya hayana madhara yoyote,” alisema mkazi wa eneo hilo, Huseni
Juma.
Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi alisema mvua kubwa zaidi ya
milimita 50 ambazo zimenyesha sasa, zinatarajia kuendelea kunyesha ndani ya saa
24 zijazo huku mvua hizo kuendelea kunyesha hadi Machi 25, mwaka huu.
“Utabiri unaonesha kuwa mvua kubwa za zaidi ya
milimita 50 zitaendelea kunyesha siku tatu zijazo. Hivyo ni vema wananchi
wakaendelea kuangalia utabiri unaotolewa na mamlaka kila siku ili kujiepusha na
madhara,” alisema.
Awali, TMA ilitoa mwelekeo wa mvua za masika kwa
kipindi cha Machi, Aprili na Mei na kuwa kipindi hicho mvua zilitarajiwa kuwa
ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
Chanzo Habari Leo
No comments:
Post a Comment