CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema vitendo
vinavyofanywa na Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ni
ukiukwaji wa Katiba na kanuni za chama hicho.
Aidha, kimesema vitendo vinavyofanywa na Lowassa
ni kampeni za wazi za urais anazoendesha kabla ya muda kufika na hivyo kukiuka
Katiba na kanuni za CCM na kuonya kuwa kama ataendelea na kampeni hizo haramu
atapoteza sifa za kugombea nafasi ya urais.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alitoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari waliopo katika msafara wa
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutaka ufafanuzi wa kinachoendelea mjini
Dodoma kwa makundi tofauti kwenda kwa Lowassa kwa madai ya kumshawishi agombee
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nape akizungumzia suala hilo alisema,
“Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi, ni matendo ya wazi ya
kampeni, bila shaka anajua adhabu yake. Matendo hayo yanaweza kumpotezea sifa
za kuwa mgombea kupitia CCM.”
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa
aliongeza kuwa Lowassa ni miongoni mwa wanaCCM ambao walipewa adhabu na CCM
mwaka mmoja uliopita kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na mpaka sasa bado wapo
kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi
yao.
Nape alisisitiza kuwa matendo yanayoendelea hivi
sasa ni dhahiri kuwa ni kiburi kisicho na maana dhidi ya CCM.
“Lowasa anajua utaratibu wa Chama katika
kuwapata wagombea wake kwa ngazi mbalimbali kuanzia udiwani mpaka urais hivyo
kuendelea na matendo ambayo yanatafsiri ya wazi kuwa ni kampeni ni kiburi cha
wazi. “Kwa matendo hayo ya Lowassa labda dhamira iwe ni kuomba ridhaa ya
kuwania nafasi ya Urais kupitia chama kingine na si CCM.”
Nape alisema ni vyema wagombea wa ngazi
mbalimbali wakahakikisha wanazingatia Katiba na kanuni za chama hicho ili
wasiingie kwenye kundi la kutokuwa na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea
udiwani, ubunge na urais.
“Tunaendelea kukumbusha na kusisitiza kwamba
wale wote wenye nia ya kugombea kupitia chama chetu kuheshimu kanuni na
tararibu za kupata ridhaa kugombea kwa ngazi ya chama chetu,” alisema
Nape.
Lowassa amedaiwa kuwa amekuwa akitumia makundi
mbalimbali kufanya kampeni ambapo alianza na kikundi cha wajasiriamali jimboni
Monduli mkoani Arusha ambapo walienda nyumbani kwake kumuomba
agombee.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mashehe 50 kutoka
wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambao nao walikwenda nyumbani kwa Lowassa
Dodoma kwa lengo la kumshawishi agombee urais.
Baadaye walifuata wachungaji ambao nao walifunga
safari hadi nyumbani kwa Lowassa Dodoma na kusema wameamua kumuomba Lowassa
agombee urais kwa madai kuwa ana maono makubwa dhidi ya Tanzania.
Baadhi ya wachungaji hao walimwambia Lowassa
wanaamini kuwa yeye ndio chaguo sahihi kwao na ndio maana wameamua kufunga
safari na kumshawishi huku wakieleza kuwa kila mtu ametumia nauli yake kufika
Dodoma.
Kwa upande wake Lowassa, akizungumza na
wachungaji hao waliofika nyumbani kwake, alisema anafarijika kuona makundi
mbalimbali yakifika nyumbani kwake kumshawishi agombee.
Alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akisema
pia kuwa hakuna kundi ambalo analituma au kulipa fedha kwa ajili ya harakati za
kutaka kugombea urais.
Hata hivyo, tayari baadhi ya makada wa CCM ambao
wamo kwenye orodha ya kutaka kugombea urais, wametoa malalamiko yao kuwa
kinachofanywa na Lowassa si sahihi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba alisema kuwa kitendo cha kuandaa watu kwa ajili ya
kuanza kampeni si cha kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo,
lakini wanaheshimu kanuni na Katiba za chama chao.
January amenukuliwa kwenye vyombo mbalimbali vya
habari na mitandao ya kijamii akieleza wazi kuwa anaweza kutengeneza makundi
kwa ajili ya kuonesha Watanzania kuwa anahitajika, lakini akasema hizo ni
propaganda ambazo hazina tija kwa Taifa.
“Kama mgombea anakubalika kwa Watanzania kwanini
atumie fedha nyingi kutafuta makundi ili aonekane anakubalika? Alihoji January
katika ujumbe wake aliousambaza katika mitandao mbalimbali ya
kijamii.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment