Najua umenisubiri kwa hamu kubwa bi shosti, ni mimi
yuleyule mtambo wa kurekebisha tabia nimeingia kama upepo wa kimbunga. Kwa vile nia ya kona hii ni kutibu si
kubembeleza watu wala kuangalia sura zao. Unajua kuna baadhi ya wanawake
wanatia kichefuchefu kufanya utani katika ndoa na
kuzifanya ndoa za siku hizi
zipoteze maana na kushindwa kutofautisha yupi kaolewa na yupi kahaba.
Nimebahatika kuhudhuria kicheni pati nyingi nikiwa kama
mgeni mwalikwa, nashukuru Mungu kila aliyenialika alikubali ushauri wangu. Siku
zote nimekuwa nikiwaeleza kuwa anayejua ladha ya kitu ni yule aliyekionja hata
akikielezea atakielezea kwa ufasaha zaidi tofauti na yule asiyeijua ladha
atabahatisha kwa vile alisikia tu muonjaji akielezea utamu na uchungu wa kitu
kile.
Kwa kweli bado nalia na maadili mabaya katika ndoa za
watoto wetu wa karne hii, wewe mzazi unaalika watu kuja kumfunda mwari wakiwa
hawajui nini maana ya ndoa kwa vile wamesikia basi ndiyo wanatoa mafundisho
kwamba ndoa inatakiwa hiki na hiki, kwa kukisikia na si kwa uhalisia ndiyo
maana wanakaa uchi mbele ya mwari sasa wamekuja kumfundisha mema au maovu?
Leo nataka kuzungumza na kina mama wakosa haya wasiyojua
vibaya, inawezekana kabisa ndoa yako inawaka moto kutokana na ujinga wako
kiburi kujisikia humjali mume unataka kila kitu ukipate usipopata mumeo humpi
haki ya ndoa. Leo hii wewe unamcheza mwanao na kuwaita wakosa haya wenzako mje
mumfunde mwari.
Mtamfundisha nini kama siyo wewe kuwa chanzo cha
kuiharibu ndoa ya mwanao? Hao mashoga zako wanatoa nasaha za aibu mbele ya
binti yako anayetaka kuolewa nawe upo pembeni unapiga vigelegele mtoto kaolewa
kesho kaachika mbaya nani?
Japokuwa kicheni pati si sehemu sahihi ya kumfunda mwari,
basi tutafute watu waliodumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu ili waweze kutoa
nasaha halisia wala si za kuhisia. Hata mavazi yao ni somo tosha kwa mwanao
kuonesha mwanamke anatakiwa kustiri maungo yake kwa vile mhusika wa kuyaona ni
mumewe tu.
Mbele unamsimamisha mwanamke
mwenye sifa ya kuchanganya
wanaume kama zege nguo alizovaa mwili wote upo nje na yeye anakueleza eti ndoa
ni ngumu mheshimu mumeo. Wakati yeye pengine ameachika ndoa zaidi ya tatu.
Siku zote mfano mzuri ni wa vitendo si wa maneno,
anayekufunda ukimuangalia kweli anachokisema ndicho anachokifanya. Kwako
unamchukulia kama mfano wako katika maisha ya ndoa, ili ukiteleza basi
umkimbilie mara moja kukupa mungozo wa
ndoa yako ili ujue umejikwaa wapi na ufanye nini.
Kingine wazazi sisi ndiyo tunatakiwa kuwa viongozi wa
watoto wetu waipende ndoa kupitia maisha yetu ya ndani ya wewe na mumeo. Ndani
ya nyumba hamzungumzi au mama anamdharau baba. Pale unamfundisha nini mwanao
ina maana na yeye atajua kumbe kumdharau mwanaume ni jambo la kawaida na ni
haki ya msingi.
Kama kweli tuna nia nzuri na watoto wetu basi sisi ndiyo
walimu wa kwanza kuhakikisha ndoa zao zinadumu. Tujiepushe kuwashirikisha watu
wasiojua thamani ya ndoa, kila aliyeionja ndoa ataielezea kwa ufasaha zaidi ili
muolewaji basi apate faida na kujiandaa vizuri katika ndoa yake.
Wazo langu jipya ambalo najua litakushtua lakini kama
wazazi mtalifanya hili basi nina imani watoto wenu wa kike watapata faida kubwa
katika ndoa zao.
Muda ukikaribia mtoto wako wa kike kuolewa kama hakupitia
unyago mweke chini ukiwa na shoga zako waliodumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu
mwelezeni ndoa ni nini, utamu na uchungu wa ndoa ambao wote umebebwa na upendo,
heshima, adabu, huruma na uvumilivu.
Nina imani somo hili likifanyiwa kazi, tutafanya ndoa
zipate heshima kuliko kuwaita wahuni kutukana mbele yamwari wetu.
Chanzo: Global publishers
No comments:
Post a Comment