Utaijua
bustani yenye afya wakati unapoiona: laini, kama vile ni zulia la kijani
limetandikwa chini, ukitembea humo hamna majani makavu yanayojaa miguuni
kukufanya uchafuke miguu na viatu vyako.
Sasa, kwavile bustani yako haionekani
hivyo umeamua kuiboresha au labda ndio kwanza unafikiria kuanzisha mpya. Kipindi hiki cha mvua ndicho kinafaa zaidi kwa
shughuli za kuanzisha au maboresho ya bustani.
Kupata
muonekano maridhawa wa bustani inatakiwa ubadili fikra zako, anasema mtaalamu
na mbunifu wa bustani Hadija Adam. “Unajua jinsi wanavyosema utamu wa ngoma
uingie ucheze? Vyema, unatakiwa ugeuke ukoka. Unatakiwa ufikiri ni nini ukoka
unahitaji,” anasema Hadija.
Vitu
vya msingi anasema ni vya kawaida sana: jua, maji na mbolea. Ukishapata hivyo
hapo ni furaha tu - kwako na kwa bustani yako.
Kuanzisha
bustani mpya ni mchakato wa raha na changamoto pamoja. Inabidi maandalizi na
mipango. Unatakiwa kuandaa eneo kwa kuondoa magugu yote na kujaza udongo kama
itahitajika. Sasa hapa nikisema kujaza udongo kumbuka sio kila udongo unafaa.
Bi Adam anasema hatua ya muhimu sana ambayo watu wengi wanaruka ni hii ya
kujaza udongo. Ni muhimu sana kuweka udongo unaofaa na mbolea ya ng’ombe (sio
ya kuku kwa kuwa ina tindikali kali kwa hivyo haifai kwa kuoteshea ukoka). Bi
Hadija anashauri kama kiasi cha udongo ni robo tatu basi mbolea iwe robo.
Katika kuchanganya na kusawazisha kwa kureki usilazimishe sana tambarare
fuatilia ardhi ilivyo na mwelekeo wa maji ili usijesababisha kuweka dimbwi
kwenye bustani yako wakati wa masika. Kuwa makini sana kwa kuwa ukishaotesha
ukoka wako hutarudi nyuma tena na kuanza kung’oa kwa ajili ya makosa
yaliyofanyika mwanzo.
Kuna
aina nyingi za ukoka (majani) unazoweza kuotesha kwenye bustani yako. Nyingine
ni laini na nyembamba sana (fikiria uwanja wa golfu na wa mpira wa miguu),
wakati ukoka nyingine unaweza dhania umekanyaga nyasi kavu miguuni. Majani kwa
ajili ya bustani ni mengi na yanaendelea kugundulika mapya. Kwa majani haya
yote hali ya hewa inachangia unawiri wake.
Ieleweke
kuwa ili kuweza kupata zulia zuri la ukoka lililofunga kila mahali kwa wakati
mmoja ni kwa kuotesha mbegu kila mahali wakati wa mwanzo. Ni gharama hasa kama
unataka kufunga eneo kubwa, badala yake kununua mbegu chache ukaotesha kitalu
ndipo uanze kujipatia mbegu zako kwenye kitalu hicho. Hii ni kama kununua mbegu
za kuweza kutosha eneo lako ni gharama sana.
Kipindi
cha mvua pia ukoka wa bustani unakua kwa kasi, kwa maana hiyo unahitajika
kukatiwa. Inapokuja kwenye swala la kukata ukoka wa bustani wenye nyumba wengi
wanashindwa kujua urefu sahihi. “Watu wengi wanakata ukoka wao kwa kuuacha
mfupi sana, kitu ambacho kinayasababishia majani msongo,” anasema Bi Hadija.
Anashauri usetie mashine ya kukatia
kwenye alama ya juu au ya kati ila sio ya chini. Majani yakibaki marefu
yanafanya mizizi ikue vizuri na pia inasaidia ardhi isichomwe na jua la moja
kwa moja na kuwa kavu kwani utaingia gharama ya kuongeza umwagiliaji. Na
usiamini kuwa ukiacha majani yawe marefu ina maanisha kuyakata mara kwa mara
kila baada ya muda mfupi, anasema Hadija. Hapana, “kuna upotofu kwa watu wengi
kuwa kama wakiyakata yakawa mafupi hautakata mara kwa mara, huu ni uongo;
yanaota haraka mno kiasi kwamba hayakupunguzii muda wowote wa kukata tena”
anasema Hadija.
Kanuni
ya msingi ya bustani yoyote ile ni maji na ndio maana kwa kipindi hiki cha mvua
ni wakati uliokubalika. Maji ya kuzama yanasaidia mizizi kupenya kina kirefu
ardhini, wakati maji kidogo kidogo kila
siku yanasababisha vishina kukauka na kuzalisha majani makavu (ambayo ndio
yanachafua miguu). Kumwagilia kwa kina pia kunafukuza wadudu wanaojishika
kwenye majani. Kwa bustani mpya iliyooteshwa ukoka mwagilia maji mengi kila
siku hadi mizizi ishike. Mizizi ikishashika ndio unaendelea kumwagilia kila
baada ya siku mbili kwa kipindi kisichokuwa na mvua.
Bustani,
hata ile unayoiona ina afya inahitaji chakula imara na hewa. Chakula cha
bustani ni mbolea, mara mbili au tatu kwa mwaka wakati wa masika Hadija anashauri
ndio wakati wa kuiwekea bustani mbolea. Kwa wakati huu mbolea ya kuku ndio
inafaa zaidi hasa kuweza kutunza kile kijani cha ukoka.
Wakati
wa mvua vile vile mimea mingi inashamiri, kwa hivyo magugu kwenye bustani yako
nayo hayabaki nyuma. Njia nzuri ya kuangamiza magugu kwenye bustani ni kuchagua
ukoka unaofunga kiasi kwamba utayazuia magugu kushamiri. Yale machache
yatakayopenya dawa yake ni kuyang’olea.
Haya
sasa wewe unayetaka kuanzisha bustani au kuboresha iliyopo, wakati huu wa mvua
ndio wakati uliokubalika. Changamka!
No comments:
Post a Comment