Thursday, March 19, 2015

MUUGUZI PILI AMIRI ALIYDAIWA KUTEKWA APATIKANA....WATEKAJI WAMUAMURU AKIMBIE BILA KUGEUKA

Muuguzi wa Hospitali ya Mwananyamala, Pili Amiri aliyetekwa Machi 12, amepatikana usiku wa kuamkia jana baada ya watekaji hao kudaiwa kumtupa katika pori moja lililoko Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mwananchi lilishindwa kufanya mahojiano na muuguzi huyo jana kwa kuwa alikuwa akihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, kuanzia saa nne asubuhi hadi mwandishi alipoondoka kituoni hapo saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa shangazi yake Pili, Fatuma Mbasa, muuguzi huyo alirudi nyumbani saa 10 alfajiri jana akiwa katika hali ya kulewa na makovu kadhaa shingoni.
“Inaonekana walimpa dawa za kulevya kwa sababu alikuwa kama teja, hajiwezi na ana majeraha kadhaa na alikuwa akilalamika kuwa na maumivu shingoni,” alisema Mbasa.
Alisema licha ya kuwa Pili alikuwa hawezi kuzungumza vizuri, lakini alisema watekaji hao walimpa mateso makali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema Pili pamoja na watu wengine saba wanahojiwa kuhusu tukio hilo.
“Kuna mambo mengi tumeyagundua kuhusu utekaji huu, lakini tutayaeleza baada ya kuwa tumeshawahoji. Ingawa amepatikana lakini hatuwezi kutoa ripoti nusu nusu,” alisema Wambura na kuongeza:
“Matukio ya utekaji yapo, sisi kazi yetu siyo kulifanyia kazi tukio hili moja, lakini tutahakikisha kupitia tukio la pili, tutajua kwa kina mchezo unavyofanyika na kuuzuia ili usijirudie tena.”
Mjomba yake Pili, Amiri Kangile alisema siyo kwamba familia hiyo ni ya watu wenye uwezo wa kifedha lakini waliamua kutoa kiasi hicho cha fedha kwa watekaji ili kumuokoa ndugu yao.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya awali ya Pili, watekaji hao walikuwa wakimwamuru akatoe fedha katika akaunti yake ya NMB akiwa chini ya ulinzi mkali.
“Anasema walikuwa wakimsindikiza mpaka kwenye ATM na kumsimamia ili atoe fedha na kisha kumfunga tena kitambaa na kuondoka naye kusikojulikana,” alisema.
Kangile alisema kwa mujibu wa Pili, watekaji hao walimtoa katika pori ambalo halifahamu na kumfikisha kwenye barabara kubwa na kumuamuru akimbie bila kugeuka.

No comments:

Post a Comment