Watu wasiojulikana wamemteka Muuguzi wa Hospitali ya
Mwananyamala, Pili Amiri, huku wakitoa sharti la kupewa Sh5 milioni ili
wamuache huru.
Pili, mwenye umri wa miaka 26, alitekwa akiwa nyumbani
kwake maeneo ya Mwananyamala Komakoma, saa tano asubuhi, Alhamisi wiki
iliyopita na kuingizwa katika gari linalodaiwa kuwa ni la watekaji hao.
Akizungumzia tukio hilo, mjomba wa Pili, Rahim Kangile
alisema watekaji hao baada ya kumteka walipiga simu kwa kutumia namba ya Pili
wakidai kutumiwa kiasi hicho cha fedha.
“Waliposema wanataka Sh3 milioni, ili wamuache,
tuliwatumia lakini hawakufanya hivyo hadi jana, wakasema tuwatumie tena Sh2
milioni, tumetuma leo(jana) lakini mpaka sasa hakuna chochote tulichofanikiwa,”
alisema.
Kangile alisema watekaji hao walitoa vitisho kuwa endapo
malipo hayo hayatafanyika basi watafanya jambo lolote baya kwa muuguzi huyo.
“Tulipoona wanatoa vitisho tuliwatumia hizo hela lakini
hawajafanya chochote la kuonyesha watamuachia Pili,”alisema.
Alisema watekaji hao walitaka fedha zitumwe katika
akaunti ya NMB ya Pili, jambo ambalo lilitekelezwa na baadaye ikabainika kuwa
miamala kadhaa imefanywa kupitia mtandao wa ATM kutoka kwenye akaunti ya
muuguzi huyo.
Akizungumzia iwapo Pili alikuwa na maadui, Kangile
alisema hawana chembe ya shaka kama muuguzi huyo alikuwa na ugomvi na watu hadi
kufikia hatua ya kumteka.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophiniasis
Ngonyani alisema “ni kweli huyu muuguzi wetu ametekwa tangu Alhamisi
iliyopita, tumezipata taarifa kutoka kwa ndugu zake, baada ya kutokuonekana
nyumbani kwa siku kadhaa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa mjomba wa wanafamilia, siku moja
baada ya watekaji kumteka msichana huyo, walipiga simu wakitaka kupewa kiasi
cha Sh3 milioni.
Dk Ngonyani alisema polisi wameshapewa taarifa za tukio
hilo na wanaendelea kufanya kazi yao ili kupata taarifa za ndani zaidi.
Kamanda wa Polisi, mkoa wa kipolisi wa Kinondoni,
Camillius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka sasa
hawana uhakika kama ni utekaji au nesi huyo ametoweka katika mazingira ya
kutatanisha.
Wambura alisema polisi wanafanya uchunguzi kujua alipo
muuguzi huyo kwani bado kuna utata kuhusu namna alivyotoweka nyumbani na
mazingira ya tukio hilo yalivyokuwa.
“Kwa sasa hatuwezi kujua kwa kina kama ni utekaji au la,
tukipata taarifa zote kwa kina tutaeleza. Hatuwezi kuthibitisha kama ni utekaji
kwa sababu sisi hatujazungumza na watekaji zaidi ya kupata taarifa ya nesi huyo
kupotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema RPC Wambura.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, muuguzi
katika hospitali hiyo alisema Pili ni yatima na wengi hawakuwa wakiwafahamu
ndugu zake wa karibu, jambo linaloweka utata zaidi kuhusu nani aliye nyuma ya
utekaji huo na sababu za utekaji.
“Ana rafiki yake wa karibu hapa hospitali na huyo tu
ndiyo tunamjua, sijawahi kusikia kuwa ana ugomvi na mtu au amefanya tukio la
ajabu, kila mtu anashangazwa na hili tukio la kutekwa kwa Pili,”alisema.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment